RC Makonda Alivyo Mwaga Machozi kwa Mara Nyingine Akiombewa Kanisani

RC Makonda Alivyo Mwaga Machozi kwa Mara Nyingine Akiombewa Kanisani
Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Mhe. Paul Makonda jana  Novemba 4, 2018 aliangua kilio kwa mara nyingine kanisani aliposhiriki ibada ya Jumapili kwenye Kanisa la Efatha lililoko Mwenge jijini Dar es Salaam.

Kiongozi huyo wa Jiji la Dar es Salaam aliangua kilio hicho baada ya kupewa nafasi na Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Josephath Mwingira ya kuwasalimia waumini.

Baada ya salamu, Makonda alianza kwa kueleza kuwa lengo la kufika kwake kanisani hapo ni kuwaomba waumini wa kanisa na mchungaji wake, kumsaidia kimaombi katika vita dhidi ya vitendo vya ushoga, usagaji na matukio mengine maovu yanayoendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema siri ya ushindi wake katika vita zote ambazo amekuwa kupambana nazo ni kumtegemea Mungu, akieleza kuwa anaamini hata katika vita hiyo atashinda kwa sababu amemkabidhi Mungu.

"Jambo ambalo ninaomba kwako mtumishi (Mwingira) pamoja na kanisa, wiki hii nimefikiria mambo mengi sana, pamoja na kwamba tunafanya kazi na kusimamia sheria lakini tunasahau kwamba na Mungu yupo," alisema Makonda na kuongeza: "Tunaweza kuwa na bidii sana ya kuhakikisha tunafanya mambo mazuri ya kumpendezesha Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, lakini tukasahau Mungu ambaye hutupa nguvu na uwezo wa kufanya kazi hizo.

"Utaonekana umefanikiwa, umefanya kazi nzuri, lakini je, umefanya kazi ambayo Mungu alitaka ufanye ya kumpendeza?"

Alisema kuwa pamoja na kufanya kazi ya serikali, kwa upande mwingine anapaswa kuhakikisha mkoa wake unakuwa ni sehemu safi na salama na kumpendeza Mungu kwa kuhakikisha hakukithiri maovu.

“Na ndiyo maana niliamua kuingia kwenye vita hata ya dawa za kulevya, ninyi mnajua kwamba ukipewa madaraka ya uongozi, Mungu anakutazama kwanza wewe kama ambavyo sasa hivi Mungu akiitazama Tanzania anamwona Rais John Magufuli, ndivyo ambavyo akiutazama Mkoa wa Dar es Salaam, anamwona Makonda," alisema.

“Mungu akinitazama anaangalia ushoga unaongezeka, akiangalia anaona mateja barabarani nao wanaongezeka, unafikiri Mungu atakuwa na furaha na mimi? Ndiyo maana nimekuja kuomba ‘toba’ kwa ajili ya mkoa wangu," alieleza zaidi Makonda huku akibubujikwa na machozi.

Makonda alidumu katika hali hiyo ya kububujikwa na machozi kwa takribani robo saa 15 na aliendelea kuzungumza katika hali hiyo, akiomba msaada na nguvu ya Mungu katika kufanikisha vita hiyo ya kuhakiksha Dar es Salaam inakuwa salama.

“Eee Mungu naomba toba kwa ajili ya mkoa wangu, nahitaji uniongoze, nahitaji nguvu, sheria zipo lakini watu hawaziangalii, watu wanafanya uzinzi wala hawaogopi, nahitaji mkono wa Mungu," sauti ya Makonda ilisikika akisali kanisani hapo.

Baada ya kuanza kubugujikwa na machozi Makonda alipiga magoti, jambo ambalo lilimwinua Mchungaji Mwingira ambaye alianza kumwombea akishirikiana na waumini wake.

Katika maombi yake, mchungaji huyo alisema amebaini kiongozi huyo alikuwa anakabiliwa na makundi matatu ambayo yalikuwa yamepanga njama kumwangamiza.

“Siyo rahisi kwa kiongozi wa serikali kumwaga machozi mbele za watu, Mungu amesikia kilio chako, hata kama kulikuwa na makosa uliyoyafanya Mungu amekusaheme kwa sababu yeye husamehe," alisema Mwingira akiwa amemgusa kichwani Makonda.

“Na nimebaini kwamba kulikuwa na makundi matatu ambayo yalikuwa yamepanga njama ya kukuangamiza, lakini kwa maombi haya utakuwa salama, ulinzi wa Mungu uko juu yako."

Baada ya kufanyiwa maombi katika kanisa hilo, Makonda alikwenda katika Kanisa la Victory Chiristian Center Tabernacle (VCCT) lililopo Kawe jijini ambako pia alimwomba mchungaji na waumini nao washirikiane naye katika maombi juu ya vita hiyo ya kuisafisha Dar es Salaam.

Makonda alisema vita hiyo aliyoianzisha ni ya Watanzania wa dini zote na si yake pekee, hivyo akaomba washirikiane naye.

 “Nataka ifike mahali hata wachawi waogope kukaa katika Mkoa wa Dar es Salaam, tunataka mkoa huu ubaki salama kwa ajili ya shughuli za kibiashara tu na si uhalifu wala uovu wa aina yoyote.

Na kwa taarifa nilizonazo ni kwamba tayari baadhi ya mashoga wameanza kukimbia kwenda nchi za jirani na mikoa mingine," alisema Makonda.

Wakati wa kampeni yake ya kupambana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya, Makonda alilia hadharani Machi mwaka jana kwenye Kanisa la KKKT Kimara jijini  Dar alikokuwa akishiriki ibada ya Jumapili.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Huo ni unafiki kabisa sio uwema wa wananchi anawateget watu fulani kama kwenye madawa ya kulevya akawatangaza wake na Mbowe na kwenye watoto waliotelekezwa na baba zao akamutangaza Lowasa unakuta kesho atamutangaza wake na Zito Kabwe na Tundu Lissu kwenye orodha yake Makonda adhibitiwe kabisa maamuzi yake ni ya Kijinga sio ya kidiplomasia

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad