Chama tawala nchini Marekani cha Republican kinachoongozwa na Rais Donald Trump kimeendelea kupoteza wawakilishi (Viti) katika bunge la Congress kwenye uchaguzi mdogo unaoendelea nchini humo.
Mpaka sasa majimbo 411 yametangaza matokeo, ambapo Democrats wanaongoza kwa viti 218 huku Republicans wakifuatia na viti 193, huku matokeo mengine ya majimbo 34 ya uchaguzi yakitarajiwa kutangazwa baadae.
Hata hivyo, Chama cha Republicans kimeendelea kufanya vizuri kwenye matokeo ya uchaguzi wa Magavana na viti vya bunge la Seneti.
Kwenye uchaguzi kama huu mwaka 2014 Republicans waliibuka kidedea kwa viti 247 huku Democratic wakiambulia viti 188.
Kwa upande wa Bunge la Seneti mpaka sasa kati ya majimbo 96 yaliyotangaza matokeo, Republican wameshinda 51 na Democrats 43. Bado majimbo manne hayajatangaza matokeo.
Ushindi wa Democrats katika bunge la Congress, utamfanya Rais Trump apate upinzani mkubwa katika kutekeleza sera zake kwa miaka miwili iliyobaki ya uongozi wake.
Katika upande wa Magavana, tayari majimbo 45 yameshatangaza matokeo huku Republican wakiongoza kwa kuwa na viti 25 na Democrats 20. Bado kuna majimbo matano hayajatangaza matokeo. Mwaka 2014 Republicans walishinda majimbo 37 na Democrats 17