Rostam Aongeza Mzuka Yanga Baada ya Rais Kumtega


MANENO machache ya mfanyabiashara Rostam Aziz aliyosema jana mbele ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kuhusu Yanga yameamsha furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo ya Jwangani.

Mfanyabiashara huyo alikwenda Ikulu na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli na kuelezea mwenendo mzuri wa nchi na jinsi Rais anavyojenga uchumi wa kudumu.

“Nimekuja kumuona Rais wangu na mwenyekiti wangu wa Chama cha Mapinduzi, nimekuja kumpongeza kwa kazi nzuri anazofanya, namtakia kila la kheri,” alisema Rostam.

“Kama mfanyabiashara, naona kinachofanyika hivi sasa ni kutengeneza misingi ya uchumi ambao utakuwa kwa uhakika zaidi, yaani kwa maana ya lugha ya kiuchumi tunasema tunaondosha ‘distortion’ (uvurugaji) ili pawe na uwanja sawa watu waweze kufanya biashara zao kwa uhuru, kwa haki na hivyo ndivyo uchumi utakavyoweza kukua kuliko ilivyokuwa huko nyuma.”

Baadaye Rais Magufuli alimuuliza mfanyabiashara kama ni shabiki wa Yanga au Simba na yeye akajibu ni Yanga.

Jibu hilo limewavutia mashabiki wengi wa Yanga ambayo kwa sasa iko kwenye mvutano mkubwa kuhusu uchaguzi wa kuziba nafasi za viongozi waliojizulu.

Wakati wengine wakichukulia suala hilo ni la kawaida, lakini baadhi ya mashabiki Yanga wanadhania swali la Rais Magufuli lilikuwa na maana kubwa juu ukizingatia klabu hiyo kwa sasa haina mwenyekiti.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, aliamua kujiuzulu pamoja na makamu wake Clement Sanga na wajumbe wengine wanne, hivyo Serikali kupitia Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuagiza ufanyike uchaguzi wa kuziba nafasi hizo zilizoachwa wazi.

Mashabiki wengi wanaamini kwamba kitendo cha Rostam kuweka wazi ushabiki wake kwa Yanga huenda ukatuliza upepo wakiamini kuna neema inanukia.

Mfanyabiashara huyo aliwahi kuhusishwa na mpango wa kuwekeza kwenye klabu hiyo miaka ya nyuma.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad