MSHAMBULIAJI wa KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Ally Samatta, amempa ‘mchongo’ kiungo mshambuliaji wa Difaa El Jadida ya Morocco, Simon Msuva kuhakikisha anayafikia malengo aliyojiwekea ya kusonga mbele zaidi katika soka kwa kuondoa vile vitu vinavyomfanya asifanye vyema na kujiboresha zaidi.
Samatta kwa sasa ndiye kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Ubelgiji kwa kuwa na mabao 10 huku akielezwa kuwa anazivutia timu kadhaa kutoka England ikiwemo Everton, West Ham United na Leicester City, hivyo amemuonyesha mlango wa kupitia Mtanzania mwenzake huyo.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Msuva alisema Samatta amekuwa akimsihi na kumuelekeza mara kadhaa juu ya kuendelea kujituma na kujiimarisha ili aweze kuwa bora zaidi.
“Nimefurahishwa na kasi ya Samatta kama kaka yangu aliyenitangulia katika safari ya soka la kulipwa na mimi ndiyo kwanza nina mwaka mmoja, amekuwa mshambuliaji mzuri ambaye kwake kumalizia ndiyo kila kitu jambo ambalo ndivyo mshambuliaji anavyotakiwa kuwa.
“Tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara na kunieleza vitu vingi vya kufanya kwa kuangalia jinsi ninavyocheza huku akinielekeza baadhi ya vitu kuacha na vingine kuviongezea pindi ninapokuwa uwanjani ili niweze kuimarisha kiwango changu kiwe bora na kufikia mafanikio, jambo ambalo nalifanyia kazi,” alisema Msuva.
Msuva alijiunga na Difaa Julai, mwaka jana akitokea Yanga kwa dau la dola 100,000 (Sh 222m) na kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji tegemeo ndani ya kikosi chake.