Klabu ya Simba imemfuata mlinzi wake wa kushoto, Shomari Kapombe ambaye alikuwa kambini na timu ya taifa 'Taifa Stars' kufuatia kupata majeraha katika mguu wake.
Uongozi wa Simba kupitia kwa Mwenyekiti wake, Swedi Mkwabi umethibitisha kuwa mchezaji huyo amepelekwa hospitali kufanyiwa vipimo zaidi baada ya kuumia akiwa mazoezini na Taifa Stars, wakati ikijiandaa na mchezo dhidi ya Lesotho uliochezwa Jumapili iliyopita.
Taarifa ya klabu hiyo iliyotolewa kupitia mitandao yake ya kijamii, imesema, "Beki wetu Shomari Kapombe leo amesafirishwa na Mwenyekiti wetu, Swedi Mkwabi kwenda jijini Cape Town, Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa vipimo zaidi baada ya kuumia mazoezini akiwa kwenye timu ya Taifa (Taifa Stars)."
Katika mchezo wake dhidi ya Lesotho wikiendi iliyopita, Taifa Stars ilipoteza nafasi ya kufuzu moja kwa moja michuano ya mataifa ya Afrika baada ya kufungwa bao 1-0 ugenini.
Kufuatia majeraha hayo, ni wazi sasa Shomari Kapombe ataukosa mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika, mchezo ambao Simba itapambana na Mbabane Swallows mwishoni mwa mwezi huu jijini Dar es salaam.