Spika wa Bunge Job Ndugai amemsifia Mbunge Ester Bulaya wa Bunda Mjini kupitia CHADEMA


Spika wa Bunge Job Ndugai amemsifia Mbunge Ester Bulaya wa Bunda Mjini kupitia CHADEMA; kwa kuibua hoja ya Makato ya 75% kwa Wastaafu yaliyowekwa na Serikali ya Magufuli

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Spika wake Job Ndugai, limejivua lawama juu ya Kanuni mpya ya pensheni ambayo imetangazwa hivi karibuni ya mstaafu kulipwa asilimia 25 ya mafao yake baada ya ukomo wa ajira.

Kanuni hiyo iliyotangazwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) pia inabainisha kuwa katika kiasi cha fedha kinachobaki, mstaafu huyo atalipwa kama mshahara kwa miaka 12.

Kutokana na suala hilo ambalo limeibua mjadala mzito kila kona huku wananchi na baadhi ya wanasiasa wakipinga, Spika wa Bunge, Job Ndugai, jana aliibuka na kuweka bayana ukweli huku akisema Bunge halihusiki katika suala hilo.

Sambamba na kuweka wazi suala hilo, Ndugai pia alisema bunge linaweza kuingingilia na kuagiza kanuni hiyo ifanyiwe mabadiliko kama inaonekana ni kandamizi.

Akizungumza na Nipashe Jumapili kwa njia ya simu, Ndugai alisema kanuni hiyo ambayo inalalamikiwa haijatokana na chombo hicho cha kutunga sheria kwa kuwa kazi ya kutunga kanuni ni ya serikali kupitia wizara husika na sheria iliyopitishwa.

“Hii si sheria bali ni kanuni na kwa kawaida bunge lilishatunga sheria, hatua inayofuata ni kupelekwa kwa Rais kwa ajili ya kutiwa saini. Lakini kabla ya kuanza kutumika, wizara yenye dhamana na sekta husika inatunga kanuni na kuzitangaza katika Gazeti la Serikali,” alisema.

“Sasa kwa jambo hilo ambalo limeibua mjadala mzito, Bunge limetwishwa mzigo mzito lisioustahili na hata watu wamefikia hatua ya kunishambulia mimi binafsi. Ukweli ni kwamba katika hili, Wizara yenye dhamana na sekta ya hifadhi ya jamii (Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) ndiyo iliyotunga kanuni hiyo,” aliongeza.

Ndugai pia alimsifu Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya, ambaye pia ni Waziri Kivuli Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), aliyeibua suala hilo juu ya pensheni hiyo.

Alhamisi wiki hii, Bulaya aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kikokotoo hicho kipya kilichotungwa na serikali ni kitanzi kwa wastaafu kwa kuwa hawatanufaika na fedha zao ambazo wamezitolea jasho kwa miaka mingi.

“Kwa kweli alichokisema Mheshimiwa Bulaya ni kweli na ameweka wazi kwamba imetokana na serikali na Bunge halihusiki,” alisema.

Katika taarifa yake kwa wanahabari, Bulaya alikaririwa akisema: “Wabunge tulitaka kikokotoo kiwepo kwenye sheria, lakini kwa masikitiko makubwa bungeni tuliambiwa kuwa ni kanuni ambayo inampa waziri ambaye yuko kwa maslahi ya serikali.”

Bulaya aliongeza kuwa, hata wadau waliwataka wabunge wakijue kikokotoo hicho na waliomba kisiwe 1/580 bali kiwe 1/540 au pungufu, lakini kilifichwa na hakikujulikana kwa watunga sheria hao.

Pamoja na bunge kutowekwa wazi, kwa mujibu wa Bulaya, SSRA hivi karibuni iliweka bayana suala hilo na hatimaye kuibua mjadala mzito kila kona huku baadhi ya wananchi wakisema ni ukandamizaji dhidi ya wastaafu.

ATOA MATUMAINI

Spika Ndugai alitoa matumaini kuwa suala hilo si kwamba limefika mwisho bali Bunge linaweza kuliibua tena kwa mujibu wa kanuni yake na hatimaye kuagiza lifanyiwe mabadiliko.

“Bunge linayo nafasi ya kuingilia kati juu ya jambo hilo na lolote lile ambalo wananchi au wadau wanaona haliwatendei haki. Kamati ya Sheria Ndogo chini ya Mheshimiwa Andrew Chenge, inaweza kusimamia hilo kwa niaba ya Bunge na kukafanyika Mabadiliko,” alisema.

Ndugai alisema hatua hiyo inaweza kufikiwa iwapo mbunge ataonyesha nia ya kufanya hivyo au kupokea malalamiko kutoka kwa wadau ambao ni wananchi.

“Baada ya kufikiwa hapo, bunge kupitia Kamati ya Sheria Ndogo itachambua na hatimaye kuiagiza serikali kufanyia marekebisho. Kwa hiyo wananchi wasione kama jambo hili limefika mwisho,” alisisitiza.

MAONI YA WANANCHI

Baada ya Bulaya kuibua jambo hilo, baadhi ya wananchi walionyesha kushangazwa huku wakilitupia lawama Bunge kwa kile walichadai kuwa limetunga sheria inayokandamaiza wastaafu.

Baadhi ya wananchi hao, wakiwamo wafanyakazi waliozungumza na Nipashe jana, walielezea kushtushwa na kanuni hiyo wakiielezea kuwa ikitekelezwa itaminya haki za wastaafu hasa baada ya kazi ngumu ya kulitumikia taifa kwa muda mrefu.

Ali Dande, mkazi wa Sinza Moro, alielezea kushangazwa kwake na wabunge kukubaliana na kanuni hiyo iliyotangazwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), wakati wao wakistaafu wanalipwa kiinua mgongo chao chote, tena bila masharti.

"Leo hii hata ukikosa kazi huwezi kuchukua mafao yako hadi ufikishe miaka 60, sasa wakati bado hatujasahau machungu haya wanatuletea lingine kwamba tusilipwe mafao yetu yote tulipwe asilimia 25 tu jamani? Mimi nashauri mtu anapostaafu apewe stahili zake aende akafanye anachokijua mwenyewe maana hela ni zake si za serikali," alisema

Hellen Murya, mkazi wa Yombo Temeke, alisema atashangaa kuona kama wabunge watakaa kimya kuruhusu kanuni hiyo iendelee kutekelezwa kama ilivyo kwa sababu inakandamiza haki za Watanzania wanyonge.

"Kama wabunge wetu hawatapaza sauti kuhusu hili nitawashangaa sana na Watanzania wanawashangaa kwa sababu hiki ni kitu cha ajabu. Fedha za wanyonge zinataka kutumiwa kwenye mambo mengine kwa kisingizio cha kumlipa kidogo kidogo mshahara kwa miaka 12. Kwa nini umpangie matumizi mstaafu mafao ambayo ni stahili yake?" alihoji.

*Chanzo; Gazeti la Nipashe*

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad