Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Novemba 15, Spika Ndugai amesema orodha hiyo inatokana na mahudhurio ya wabunge na mawaziri kwenye mkutano wa 11 kuanzia Bunge la Bajeti pamoja na mkutano wa 12.
Ndugai amesema wabunge wa mwisho kabisa na mahudhurio yao kwenye mabano kuwa ni Mbunge wa Jimbo la Mpendae (CCM), Salim Turki (14%), Mbunge wa Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi (9%) na Mbunge wa Arusha mjini (Chadema), Godbless Lema (7%).
“Kwa hiyo Arusha wajue hawana mwakilishi hapa, hata leo ameingia dakika 15 na kuondoka, majina yao nitapeleka kwenye vyama vyao,” amesema Ndugai.
Kuhusu mawaziri, wa mwisho kabisa ni Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi (38%), Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira, January Makamba (37%) na wa mwisho ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga (35).
“Orodha hii inahusu vikao vyote vya kamati na bunge, unakuta kamati inakaa hakuna waziri wala naibu wake, na wala hakuna taarifa,” amesema Ndugai.