Tabora Waaswa Kuacha Kufungasha Asali Kwenye Chupa za Konyagi

Kamati ya maandalizi ya Jukwaa la Fursa za Biashara Tabora imetoa mwito kwa wananchi mkoani humo wajipange ili jukwaa hilo lisiwaache kama litakavyokuta.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Tabora, Rukia Manduta amesema mjini Tabora kuwa, jukwaa hilo ni kwa ajili ya wananchi wa mkoani humo na ndio watekelezaji.

Ameshazungumza hapa mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, tuache kufungasha asali kwenye chupa za konyagi, karanga kwenye plastiki, makaratasi ya plastiki, basi tukiwanao pale tunaweza tukawapata watu wadau ambao wanaweza wakaanza kututengenezea vifungashio na bidhaa zetu ziwe bora," amesema.

Manduta amesema, Novemba 22 kutakuwa na mawasilisho kwenye ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi, na kwamba halmashauri nane za Tabora, mkoa na taasisi watawasilisha fursa walizonazo. Amesema, Novemba 23 kutakuwa na maonesho tena ya wajasiriamali na wafanyabiashara.

Kama alivyosema Mkuu wa Mkoa mgeni rasmi atakuwa mheshimiwa Waziri Mkuu, sio ugeni mdogo, ni ugeni mkubwa sana, na watakuja watu wengi, tunawasihi watu wa Tabora kuwa watu bora kwa wageni wetu watakaofika, waonyeshe wajisikie kwamba tumekuja Tabora tumekutana na watu bora sio wamekuja Tabora wamekutana na bora watu, watu bora na sio bora watu," amesema Manduta.

Hili jambo limekuja kwa ajili yenu na ni jambo lenu kwa hiyo nataka mlichukue na mlipokee kwa mikono miwili tunaenda kusisitiza jambo lipo mbele ya uso wetu, tarehe 21, 22, 23, ni Jumatano ijayo, sio mbali. Kwa hiyo lazima mlijue hilo, mmejipangaje, jukwaa likiondoka litakuachaje, likuache kama lilivyokukuta, kwa hiyo ni maswali ambayo mnatakiwa mjiulize,"amesema Manduta.

Ametoa wito kwa wajasiriamali na wafanyabishara kutopandisha bei za bidhaa wakati wa jukwaa na pia wanaotoa huduma za usafiri na malazi wawe na utu, waaminifu na wastaarabu kwa wageni. Jukwaa la Fursa za Biashara Tabora linatarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe 400 wakiwemo wakuu wa mikoa na mawaziri.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad