Tanzania U23 Yajigamba Kuondoa Aibu ya Stars


Timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 23 'Kilimanjaro Warriors' imejipanga vizuri kuelekea mchezo wao wa marudio kuwania kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika dhidi ya Burundi hapo kesho.


Timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 23.

Mchezo huo utachezwa kuanzia saa 1:00 usiku katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam, ambapo katika mchezo wa awali Kilimanjaro Warriors ilifungwa mabao 2-0 mjini Bujumbura.

Akizungumza kuelekea mchezo huo, kocha wa Kilimanjaro Warriors, Bakari Shime amesema kuwa maandalizi yamekamilika na wanafahamu kuwa walipoteza mchezo wa kwanza, akiahidi kuwa kesho watapindua matokeo hayo.

"Tumejaribu kuwajenga vijana wetu kwaajili ya mchezo, kwasababu kukamia sana mchezo hakusaidii kitu. Kwanza kikosi kimeimarika, kuna baadhi ya wachezaji hatukuwa nao Burundi kutokana na sababu tofauti tofauti lakini sasa wote wako timamu," amesema Bakari Shime.

"Tuna wachezaji wazoefu wengi, wanacheza ligi kuu na michezo kadhaa ya kimataifa, kwahiyo naamini kabisa kwa uzoefu ambao wako nao watakuwa watulivu kwajili ya kukabiliana na mchezo huo," ameongeza.

Endapo Kilimanjaro Warriors itashinda mchezo huo, itasonga mbele katika hatua nyingine ya kufuzu michuano hiyo ya AFCON itakayofanyika nchini Misri mwaka 2019.

Wakati timu hiyo ya vijana ikijiandaa na mchezo wake wa marudio, kaka zao ambao ni timu ya taifa 'Taifa Stars' imepoteza nafasi ya kufuzu moja kwa moja kwenye michuano ya AFCON nchini Cameroon kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Lesotho wikiendi iliyopita.

Katika mchezo huo, Stars ilihitaji alama tatu ili kuweza kufuzu moja kwa moja, ikiungana na Uganda ambayo tayari imeshafuzu. Sasa itasubiri hadi mechi ya mwisho ili kujua hatma ya nafasi yake, ikitakiwa kushinda dhidi ya Uganda na kuiombea ushindi au sare Cape Verde itakayopambana na Lesotho.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad