Kamati ya Uchaguzi ya shirikisho la soka nchini TFF imetangaza kuanza mchakato wa uchaguzi maalum wa kujaza nafasi mbalimbali ambazo zimeachwa wazi ndani ya klabu ya Yanga.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ally Mchungahela amesema zoezi la kuchukua fomu kwa wagombea litaanza Novemba 8 hadi 13 2018.
Ameitaja tarehe rasmi ya uchaguzi huo, ambayo ni Januari 13 2019 huku akisisitiza kuwa TFF imechukua uamuzi huo mara baada ya Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuwataka wausimamie wakieleza kuwa kamati ya Yanga haijitoshelezi.
BMT waliitaka TFF itimize majukumu hayo katika kikao na wanahabari kilichofanyika siku chache zilizopita.
Nafasi iliyo wazi ndani ya klabu ya Yanga ni ya Mwenyekiti wa klabu baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wake, Yussuf Manji kujiuzulu wadhifa wake huku nafasi mbalimbali ikiwemo Katibu Mkuu wa klabu zikikaimiwa hadi sasa.