Muda wa kuendelea kuwepo kwa mcheza soka ambaye ni nyota aliyestaafu katika mchezo wa riadha, Usain Bolt katika klabu yake ya sasa ya Central Coast Mariners umefikia ukingoni.
Mchezaji huyo ambaye alijiunga na Central Coast Mariners mwezi Agosti, hajahudhuria mazoezi tangu siku kadhaa kabla ya mwisho wa mwezi Oktoba kutokana na pande zote mbili (mchezaji na klabu) kutokubaliana katika vipengele vya mkataba wake ambao aliwekewa mezani.
Uongozi wa klabu hiyo umetoa taarifa mapema leo, ikithibitisha kuwa, "licha ya jitihada kubwa za ushawishi za washirika mbalimbali juu ya mchezaji huyo, muda wake wa kuendelea kuwepo hapa umekwisha".
Kwa upande wake, mchezaji huyo ambaye ni bingwa mara nane wa medali za dhahabu katika michuano ya Olympic amesema, "ninapenda kuwashukuru wamiliki wa klabu ya Central Coast Mariners, uongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki kwa kunifanya nijisikie niko nyumbani kwa kipindi chote nilichokuwa hapa".
Klabu hiyo imeanza msimu wa ligi kuu nchini Australia maarufu kama 'A-League' kwa kupata sare mbili dhidi ya Brisbane Roar na Melbourne City.
Usain Bolt alistaafu riadha mwaka uliopita na kuamua kugeukia katika soka ambako yeye mwenyewe alisema kuwa ni moja kati ya ndoto yake ya muda mrefu. Alifanya mazoezi katika klabu kadhaa barani Ulaya ikiwemo Borussia Dortmund kabla ya kuelekea nchini Australia ambako alifanikiwa kuanza vizuri na klabu ya Central Coast Mariners, ikiwemo kufunga mabao mawili ya kwanza katika mchezo wake wa kwanza wa kiushindani.