Mbunge wa Chalinze na wakili wa Mahakama Kuu nchini Ridhiwani Kikwete ameonesha kushindwa kujizuia kwa kuandika maneno ya kujivunia juu ya baba yake ambaye ni Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete baada ya kiongozi huyo kutangazwa kuwa ni miongoni mwa mfano wa viongozi bora.
Hatua hiyo ya Ridhiwani imekuja kufuatia Rais huyo mstaafu kutunukiwa tuzo na taasisi ya Women Advacement for Economic and Leadership Empowerement Foundation (WAELE), kutokana na kutambua mchango wake katika masuala ya uongozi kwa wanawake.
Kupitia mitandao yake ya kijamii Ridhiwani ameandika “maneno hayatoshi kueleza furaha ninapoona , mfano wa kiongozi bora kutokea mie ninamuita baba, ninaendelea kujifunza kwako na ninafurahi kuwa mwanao, hongera sana kwa mafanikio mengine.”
Ridhiwani Kikwete ni miongoni mwa watoto wa Dkt Jakaya Kikwete ambao wapo kwenye nafasi ya uongozi na ambao wanatarajiwa kuwepo kwenye kitabu cha Kiongozi huyo mstaafu anachotarajia kukizindua hivi karibuni, alichokipa jina "kutoka mwanafunzi mtembea peku hadi Rais".
Miongoni mwa vitu ambavyo vimeonekana kuwavutia kupitia kitabu cha Dkt Jakaya Kikwete ni historia yake ya kutovaa viatu mpaka pale alipotoka mafunzo ya kijadi akiwa kijijini kwao.
“Ndo ukweli wenyewe huo, tukio hilo lazima watanzania wajue hakuna mafanikio yasiyokua na mapungufu yake, msione watu wamevaa vizuri na wana mafanikio watu wakaanza kusema ameiba lazima wafate historia wajue walipotokea na sio kuongea ongea bila msingi.” amesema ridhiwani Kikwete baada ya Baba yake kusema kuwa alivaa viatu baada ya kutoka jando.