VIDEO: Bei ya Maziwa yapanda Mara Dufu, Wananchi Walalama

Dar es Salaam. Wateja wa maziwa hasa yatokayo nje ya Tanzania wameanza kuonja joto ya jiwe baada ya kushuhudia bei ya bidhaa hiyo ikipanda maradufu.

Katika maduka ambayo Mwananchi lilipita jana jijini Dar es Salaam lilishuhudia bei ya maziwa ya ujazo wa mililita 200 yakiuzwa kwa Sh1,200 kutoka Sh700.

Aidha, yale yenye ujazo wa lita moja ambayo awali yalikuwa yakiuzwa Sh3,000 hivi sasa yanauzwa kwa kati ya Sh4,000 hadi Sh5,000.

Editha Eliya, muuzaji wa duka lililopo eneo la Mabibo, alisema maziwa yote yamepanda bei, lakini ya Azam ndiyo yamepanda zaidi na upatikanaji wake umekuwa mgumu.


“Maziwa yote kwa ujumla yamepanda bei, lakini pia hayapatikani kwa urahisi katika maduka ya jumla. Nido imepanda kutoka Sh12,000 kwa kopo hadi Sh13,000 lakini inapatikana, tatizo ni maziwa ya Azam, hayapatikani,” alisema.

Muuzaji mwingine, John Khamis alisema wateja wengi hivi sasa hawachagui maziwa kama zamani, badala yake wananunua yaliyopo hasa yenye bei nafuu.

“Wengi walikuwa wanapenda maziwa ya Azam, lakini baada ya bei kupanda wachache wanakubali kununua kwa Sh4,000. Hata sisi tunanunua kwa bei kubwa kwenye maduka ya jumla, ndiyo maana baadhi ya maduka huwezi kuyakuta,” alisema Khamis.

Kuanzia Oktoba Mosi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilipitisha kanuni zilizopandisha tozo ya kuingiza maziwa kutoka Sh150 na kufikia Sh2,000 kwa lita au kilo moja, jambo ambalo linatajwa kusababisha kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.

Mkazi wa jijini hapa, Mwantum Ahmed alisema mabadiliko ya bei yamemuongezea gharama hasa za mtoto wake mdogo anayetumia maziwa.

“Nimeshangaa baada ya kutoka kazini nimekuta dada ameshindwa kununua maziwa, anasema hela haitoshi. Nilidhani analeta ujanja ikabidi niende dukani kuulizia na nikathibitisha kupanda kwa bei hiyo. Tunaonyonyesha tunaumia zaidi,” alisema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad