Vyama viwili vikuu vya upinzani vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimeungana baada ya kujiondoa kwenye muungano wa awali uliomuweka mgombea mmoja kushindana na yule anayeungwa mkono na Rais Joseph Kabila.
DR Kongo Felix Tshisekedi (Getty Images/AFP/N. Maeterlinck)
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyotangazwa siku ya Ijumaa (23 Novemba) mjini Nairobi, Kenya, sasa Felix Tshisekedi anayeongoza chama kikubwa zaidi cha upinzani cha UPDS atasimama kwa niaba ya chama chake na kile cha spika wa zamani, Vital Kamerhe.
Kwa mujibu wa shirika la habari la la Ujerumani Deutsche Welle (DW), uamuzi huu umefikiwa ikiwa ni mwezi mmoja tu kabla ya uchaguzi wa tarehe 23 Disemba kwenye taifa hilo tajiri kwa madini la Afrika ya Kati.
Tangazo hili linamaanisha kwamba uchaguzi huu utakuwa na pande tatu kuu zinazowania: Emmanuel Ramazani Shadary anayeungwa mkono na Kabila, Martin Fayulu anayeungwa mkono na viongozi wawili wakuu wa upinzani waliozuiwa kuwania urais – Jean-Pierre Bemba na Moise Katumbi, na Tshisekedi anayeungwa mkono na Kamerhe.
Tshisekedi ataka wengine wamuunge mkono
Kollage von den vier Top-Kandidaten DR Kongo
Viongozi wakuu kuelekea uchaguzi mkuu wa Disemba 23 nchini Kongo
Tshisekedi, mtoto wa kiongozi wa muda mrefu wa upinzani, marehemu Etienne Tshisekedi, alitoa wito kwa wagombea wengine wa upinzani kumuunga mkono ili washinde uchaguzi huo.
Wiki iliyopita, makubaliano yaliyofikiwa na vyama vikuu vya upinzani mjini Geneva kumsimamisha Fayulu kuwania urais kwa niaba yao yaliporomoka, hali iliyodhoofisha juhudi za kumshinda mgombea wa chama tawala, Shadary.
Makubaliano yalivunjika baada ya kukumbana na upinzani mkali kutoka kwa chama cha UPDS cha Tshisekedi, huku maandamano na machafuko yakishuhudiwa kwenye mji mkuu, Kinshasa.
Ndani ya kipindi cha masaa 24, Tshisekedi na Kamerhe, ambaye alishika nafasi ya tatu kwenye uchaguzi wa mwaka 2011, walitangaza kujiondowa kwenye makubaliano hayo.
Kabila ashutumiwa kuendeleza nguvu zake
Muungano wa kisiasa ulioundwa na Kabila kwa ajili ya uchaguzi huu uliliita tangazo hilo la Nairobi kuwa halina maana.
DRC Präsident Joseph Kabila (Reuters/K. Katombe)
Rais Joseph Kabila ashutumiwa kutaka kuendelea kutawala nyuma ya pazia
“Wapinzani daima wako hivyo. Mtu hata hajuwi anataka nini hasa,” alisema mbunge Pius Muabilu, ambaye ni mjumbe wa timu ya kampeni ya muungano huo.
“Watu wataamua. Na wanajuwa nani anaipenda nchi hii na nani haipendi,” aliliambia shirika la habari la AP.
Kama utakwenda kama ulivyopangwa, huu huenda ukawa uchaguzi wa kwanza utakaowezesha kukabidhiana madaraka kwa njia za amani.
Uchaguzi ulikuwa ufanyike mwishoni mwa mwaka 2016 na sasa ingawa Kabila anasema ataondoka madarakani, upinzani unaamini kuwa ataendelea kuimarisha nguvu zake kama Shadary atashinda.
Kabila amekuwa madarakani tangu mwaka 2001 na muhula wake ulimalizika mwishoni mwa mwaka 2016, lakini ameendelea kusalia madarakani, akidai anatayarisha uchaguzi ambao wakosoaji wake wanasema ni mbinu ya kuimarisha nguvu zake.
Vyama vya upinzani vilitumia miezi kadhaa kujaribu kuunganisha nguvu zao kwenye uchaguzi huu ambao umezusha wasiwasi katika jamii ya kimataifa, hasa kutokana na madai ya matayarisho ya wizi wa kura kupitia mfumo wa kura za kielektroniki, madai yanayokanushwa na serikali ya Rais Kabila. Congo ina wapiga kura zaidi ya milioni 40.