Kocha wa klabu ya KMC inayoshiriki llgi kuu soka Tanzania bara, Ettiene Ndayiragije, ameingia na utaratibu mpya ndani ya klabu hiyo wa kuwapokonya simu wachezaji siku moja kabla ya mchezo ili kuwapa muda wa kupumzika zaidi.
Akiongea na www.eatv.tv nyota wa timu hiyo Hassan Kabunda amekiri kuwepo kwa utaratibu huo na kuweka wazi kuwa kwa upande wao hauna tatizo kwani unawasaidia kuwaza mchezo zaidi kuliko kukutana na vitu vingine ambavyo vinaweza kuwaondolea utayari wa mchezo.
''Kila mwalimu na utaratibu wake huyu kocha wetu ana utaratibu huo na sio kwamba anatulazimisha lakini anatushauri tukae nazo kando kitu ambacho kinatusaidia sana maana unalala mapema na pia unapata muda mzuri wa kupumzika hivyo kwa upande wangu sioni ubaya'', amesema.
Aidha Kabunda ambaye amesajiliwa na KMC msimu huu akitokea Mwadui FC amesema utaratibu huo haukuwepo kwenye klabu yake ya zamani lakini yote kwa yote anaamini mwalimu Ndayiragije hana lengo baya bali anataka kuona timu yake inapata matokeo chanya.
KMC ipo katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi kuu ikiwa na alama 13 kwenye mechi 12 ambazo imeshashuka dimbani katika msimu huu ambao ni wa kwanza kwake kushiriki ligi kuu soka Tanzania bara.