Msanii aliyekuwa kwenye kundi la Yamoto Band Beka Flavour ameeleza furaha aliyoipata baada ya kujaliwa kupata mtoto wa kiume na mpenzi wake wa muda mrefu anayeitwa Happy.
Akiongea na eNEWZ Beka amesema kuwa mtoto wake amekuja kwa muda muafaka na amekuja na baraka zote kwani ni mtoto ambaye amezaliwa ndani ya ndoa kwa kuwa familia za pande zote mbili na dini zinatambua mahusiano yao wote wawili na anaishi na mama mtoto wake huyo kama mume na mke .
Hata hivyo Beka Flavour amesema "kipindi nikiwa Yamoto Band wenzangu walikuwa wananicheka wakiniita mgumba kwa kuwa nilikuwa nimewazidi umri lakini wao walikuwa wamenizidi kwa kuwa na watoto ila mimi nilikuwa na mipango yangu na kwa sasa ndio wakati muafaka niliopanga mimi na mzazi mwenzangu kupata mtoto na hakuja kwa bahati mbaya".
Pia Beka Flavour amesema kwa wale wanaomjua kwa jina la Beka Flavour waendelee kumjua hivyo na wale watakaopenda kumuita Baba Aaryan wamuite huku akisema kwamba tayari ameshamfungulia mtoto wake account katika mtandao wa instagram ambayo kwa sasa tayari ina wafuasi elfu mbili.