DC Jokate ameyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Wanawake ambapo amesema hawajahi kuamini anashindwa kufanya chochote anachoamua kufanya, kwani hilo limechangiwa na malezi kutoka kwa wazazi wake.
“Nawapa changamoto wanawake wenzangu kwani mara nyingi wanaume ni wachoyo, aidha ni wachoyo ama wanaogopa nguvu ya mwanamke, kwani mara nyingi haki zinapiganiwa na hatupewi mikononi tukamate fursa. Tujifunze na tusipende kutosheka,” amesema.
Jokate ameongeza kuwa ili wanawake wakamate nafasi mbalimbali za uongozi lazima wajifunze, wawe na ujuzi, elimu na maarifa, “Wanawake wasiogope kujitokeza kuitwa wanakimbele mbele kwani wanasema huyu aliyekuwa modo na leo mwanasiasa inahusu?, mie nawaambia inahusu kwani uwezo ninao maamuzi ninayo nitafanya kazi kwa bidii zote".
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amesema kuwa takwimu za mwaka 2017, idadi ya wanawake viongozi katika taasisi mbalimbali imeongezeka na kufikia 117, kutoka 114 ya mwaka 2014, ikilinganishwa na idadi ya wanaume ambao ilikua 526 ya mwaka 2014 na kupungua kufikia 352 ya 2017.