Dunia imewahi kushuhudia wanawake mbalimbali mahiri katika nyadhifa za kisiasa ambao matendo yao ya kiuongozi yamewahi kuwahamaisha wengine kutaka kuwa Viongozi. Huwa inatokea mara chache sana katika maisha ya mwanadamu kwa wanawake kushika nyadhifa za juu za kiuongozi katika nchi zao ila wapo wachache ambao wamewahi kushika nyadhifa hizo na wakazitendea haki. Leo tuangalie wanawake mahiri na waliothubutu kwa kushika nyadhifa ngumu na kubwa duniani.
10. Asha Rose Migiro
Tuanzie nyumbani kwa mama Asha Rose Migiro. Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Akawa ni mwanamke wa pili kushika wadhifa huo huku pia akiwa ni mwafrika wa kwanza kushika nyadhifa hiyo. Mwanadiplomasia huyo, alidumu kwa miaka mitano toka 2007 mpaka 2012. Katika kipindi cha utawala wake alipambana kuhusu haki za mwanamke hasa katika nchi zinazoendelea.
9. Yulia Tymoshenko
Huyu ni mwanasiasa toka nchini Ukraine. Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Ukraine. Kuchaguliwa huko kukamfanya awe mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo. Mwaka 2010 alijitosa kwenye Uchaguzi wa Rais wa Nchi hiyo na kuambulia nafasi ya pili nyuma ya Viktor Yanukovych ambaye aliibuka Rais kwa tofauti ya asilimia 3.5
Baada ya Uchaguzi huo, Yulia alianza kuandamwa na serikali mpya ya nchi hiyo kwa kubambikiwa makosa mbalimbali ya jinai na kuhukumiwa jela miaka 7. Baada ya shinikizo la nchi za Magharibi, aliachiwa huru mwaka 2014 na kujitosa tena kwenye mbio za Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2014 na kushika nafasi ya pili tena safari hii akiwa nyuma ya Petro Poroshenko. Mwaka huu ametangaza kugombea tena Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2019.
8. Hillary Clinton
Mwanamama huyu alikuwa ni first lady wa Marekani kuanzia mwaka 1993-2001 ambapo mumewe Bill Clinton alikuwa Rais wa Nchi hiyo. Mwaka 2009 mpaka 2013 alishika madaraka makubwa ya kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika utawala wa Rais Obama. Katika muda wake akiwa kama Waziri wa Mambo ya Nje atakumbukwa kwa operesheni za kuwaondoa madarakani baadhi ya viongozi wa Kiarabu waliokaa madarakani kwa muda mrefu kama Gaddafi na Hosni Mubarak.
Mwanamama huyo, alipambana katika kugombea nafasi ya Urais kwa mwaka 2016 lakini akaambulia nafasi ya pili nyuma ya mshindi wa uchaguzi huo, Donald Trump. Licha ya kushinda kwake, bado anachukuliwa mmoja wa wanawake majasiri katika historia ya Marekani.
7. Ellen Johnson Sirleaf
Mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Urais barani Afrika kuanzia mwaka 2006 mpaka 2018 akiiongoza nchi ya Liberia. Anajulikana kama Indira Gandhi wa Afrika akifananishwa staili yake ya uongozi na aliyekuwa kiongozi mahiri wa nchi ya India. Mtetezi mkubwa wa haki za wanawake barani Afrika hali iliyompelekea kutwaa Tuzo ya Amani ya Nishani ya Nobel kwa mchango wake huo. Uongozi wake ulileta umoja wa kitaifa katika nchi hiyo iliyopitia kipindi kigumu cha vita ya wenyewe kwa wenyewe kabla ya hapo.
Hakuupata Urais kirahisi, kwani mwaka 1980 alilazimika kukimbilia Uhamishoni chini ya utawala wa Dikteta Samuel Doe. Bibie Ellen alikimbilia Marekani kabla ya kurudi tena nchini Liberia na kugombea Urais mwaka 1997 na kuishia kushika nafasi ya pili nyuma ya Charles Taylor. Hakukata tamaa na hatimae mwaka 2005 akashinda Urais.
6. Condoleezza Rice
Anatajwa kama mwanamke wa Shoka katika utawala wa Rais George W. Bush. Kwanza kabisa, katika muhula wa kwanza ya Rais George Bush, mwaka 2001 mpaka 2005 alikuwa Mshauri Mkuu wa masuala ya Ulinzi na Usalama kwa Rais Bush, kwa wadhifa huo akawa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo katika nchi ya Marekani. Ni katika nafasi hiyo aliyoshika, vita dhidi ya ugaidi ilitambulishwa na kupelekea kuangushwa kwa utawala wa Saddam Hussein wa Iraq.
Pili, katika muhula wa pili wa Rais Bush kuanzia mwaka 2005 mpaka 2009, alichaguliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo. Alisimamia vyema na kuhakikisha vita dhidi ya Ugaidi ikiendelea na alihakikisha Saddam Hussein ananyongwa kama hukumu ilivyotoka.
Condoleeza Rice hakuwahi kuolewa wala kupata mtoto, ni mwanadiplomasia mbobezi na jasusi mahiri sana ndio maana haishangazi kuona akishika nyadhifa nyeti na muhimu nchini Marekani.
5. Angela Merkel
Ndiye Kansela wa sasa wa Ujerumani, mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo. Anatajwa kama mwanamke jasiri na mpambanji na mwenye nguvu duniani kwa sasa. Ameshika wadhifa huo toka mwaka 2005.
Aliolewa na kuachika mwaka 1982 na mwanafizikia Ulrich Merkel kabla kuolewa na mumewe wa sasa Mkemia Joachim Sauer. Licha ya kuachika na mumewe wa kwanza mwaka 1982 bado ameendelea kutumia jina la mumewe huyo (Merkel) mpaka leo.Angela Merkel hajawahi kupata mtoto katika maisha yake.
4. Benazir Bhutto
Watu wa kariba ya Benazir huwa wanazaliwa mara chache sana katika maisha ya mwanadamu.
Huyu ni mwanamke wa shoka, ameshika nafasi ya Waziri Mkuu wa nchi ya Pakistani mara mbili.
Mara ya kwanza alishika wadhifa huo ni mwaka 1988 mpaka 1990. Kwa mara ya pili alishika wadhifa huo mwaka 1993 mpaka 1996. Katika kipindi hiki cha pili cha utawala wake akiwa kama Waziri Mkuu wa Pakistani, alikuwa na sera za kumuinua mwanamke. Pia utawala wake uligubikwa na mauaji ya kaka yake aliyefahamika kama Murtaza Bhutto (Alimuua kaka yake). Pia mwaka 1995 alinusurika katika jaribio lililoshindwa la Kumpindua.
Mwaka 1997 alishindwa Uchaguzi na kuamua kwenda kuishi uhamishoni Dubai, mwaka 2007 aliamua kurudi Pakistani kwaajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2008 dhidi ya Jenerali Pervez Musharaf lakini kabla ya mwaka huo kuisha aliuwawa baada ya kutegeshewa bomu katika gari.
3. Indira Gandhi
Mwanamke pekee kushika wadhifa wa Waziri Mkuu nchini India kuanzia mwaka 1966 mpaka 1977. Kwa awamu ya pili alishika wadhifa huo kuanzia mwaka 1980 mpaka 1984 alipouwawa na walinzi wake. Kushika huko majukumu ya Uwaziri Mkuu mara mbili kumemfanya awe mtu wa pili kushika wadhifa huo kwa muda mrefu zaidi. Indira Gandhi hana undugu wowote na Mahatma Gandhi ( Baba wa Taifa wa India ).
Katika utawala wake, India iliingia vitani dhidi ya Pakistan na hii ilipelekea kuzaliwa kwa Taifa la Bangladesh. Anatajwa kama mwanamke aliyekuwa na uthubutu wa hali ya juu kwa maslahi ya Taifa lake na ndio maana haishangazi kuona mwaka 2009 alichaguliwa kuwa mwanamke wa Milenia na shirika la Utangazaji la Uingereza BBC.
2. Golda Meir
Mzaliwa wa jimbo la Kiev nchini USSR ( Kwasasa Ukraine ), kabla ya kuhamia Marekani kwa ajili ya elimu.
Golda Meir alikuwa Waziri Mkuu wa 4 wa Israel na mwanamke pekee kushika wadhifa huo mpaka sasa. Anatambulika kama "Iron Lady" wa siasa za Israel. Anatajwa kama mwanamke mahiri zaidi kuwahi kutokea katika uso wa nchi ya Israel. Kabla ya kuwa Waziri Mkuu aliwahi kuwa Waziri wa Kazi na Waziri wa Mambo ya Nje nchini humo.
Mwaka 1967 akiwa waziri wa Mambo ya Nje wa Israel ndipo kulitokea vita maarufu ya siku sita, vita dhidi y a Mataifa ya Kiarabu. Alitimiza majukumu yake na kuisaidia nchi yake kuibuka mshndi wa vita hiyo.
Mwaka 1969 alichaguliwa kushika nafasi ya Uwaziri Mkuu, cheo kikubwa zaidi nchini humo. Ni katika kipindi chake cha uongozi, mwaka 1972 kulitokea mauaji ya wanamichezo wa Israel waliokuwa wanashiriki michezo ya Olimpiki ya Majira ya Kiangazi jijini Munich nchini Ujerumani. Wanamichezo wa Israel wapatao 11 waliuwawa na kikundi cha Black September cha Palestina.
Hapo ndipo Golda Meir kama Waziri Mkuu, alipitisha na kuidhinisha "Operation Wrath of God" au Operation Bayonet ambapo aliwaagiza MOSSAD kuhakikisha waote waliohusika na mauaji ya wanamichezo wale wa Israel wanakamatwa wakiwa Hai au Wamekufa. Operation hiyo ilikuja kudumu kwa miaka 20 na ilikuja kufanikiwa kwa asilimia 100 kwani wote waliohusika walikuja kuuwawa.
Hii ilipelekea Golda Meir kunusurika katika jaribio la kuuwawa jijini Rome alipoonda kukutana na Papa Paul wa 6.
Mwaka 1974, Golda Meir alijiuzulu ghafla nafasi ya Uwaziri Mkuu kwa sababu ya vita ya Yom Kippur.
1. Margaret Thatcher
Anajulikana zaidi kama "Iron Lady" kwa matukio yake ya kisiasa yenye maamuzi magumu bila ya kuyumbishwa. Ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Uwaziri Mkuu nchini Uingereza kuanzia mwaka 1979 mpaka 1990 katika kipindi ambacho Dunia ilikuwa inapitia katika kipindi cha vita baridi.
Anajulikana kwa misimamo yake iliyomfanya wengi wamchukulie kama mwanaume, ameshika wadhifa wa Uwaziri mkuu kwa muda mrefu zaidi katika karne ya 20. Licha ya Vita baridi iliyokuwepo kati ya Kambi ya Mashariki (Urusi) dhidi ya Magharibi (Marekani, Uingereza, Ufaransa), Margaret Thatcher katika uongozi wake alikumbwa na Vita ya kugombea Visiwa vya Falkland dhidi ya Argentina. Lakini chini ya uongozi wake imara aliibuka na ushindi katika vita hiyo.
Katika utawala wake alijenga urafiki wa karibu sana na Rais wa Marekani wa kipindi hiko ndugu Ronald Reagan na ushirikiano wao ulifanikwa kuiangusha USSR katika vita baridi.
Hakuna marefu yasiyo na ncha, mwaka 1990, Iron Lady alijiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu wa nchi hiyo pamoja na ile ya Uongozi wa chama chake cha Conservative baada ya kuanza kupoteza ushawishi ndani ya nchi hiyo hali iliyopelekea kuwashtua viongozi wengi wa Dunia.
MWISHO