Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba, ameibuka na kusema kuna umuhimu wa Tanzania kuwa na katiba mpya, kutokana na uhitaji haswa kwenye masuala ya kulinda utamaduni pamoja kulea maadili ya Taifa ikiwemo usambazaji picha za zisizokuwa na maadili.
Jaji Warioba ameyasema hayo jijini Dar es salaam ikiwa ni siku chache baada ya Rais Magufuli kuzungumzia suala la katiba mpya alipokuwa kwenye kongamano la kujadili hali ya uchumi na kisiasa na kusema suala hilo sio kipaumbele chake kwa sasa.
“Kuna mambo mengine ya msingi ambayo kwenye katiba pendekezwa yametolewa, kama wakisema tukienda na hii katiba pendekezwa mimi nitakuwa wa kwanza kuipinga , na ukiangalia wanasiasa wengi wanachoangalia sana ni kuhusu masuala ya utawala.”, amesema.
“Wanachoongelea sana, matokeo ya Urais kupingwa, tume huru ya uchaguzi lakini kuna mambo ya msingi zaidi ya hayo ambayo yalinyofolewa kwenye rasimu, mfano kuporomoka kwa maadili na wananchi walikuwa na mawazo mengi kuhusu maadili.”
Aidha amependekeza kuingizwa kwenye rasimu ya katiba suala la ulinzi wa rasilimali za taifa kuingizwa kwenye katiba mpya ili kurahisisha suala hilo na kueleza suala hilo litasaidia rasilimali zilizopo kuwanufaisha watanzania.
“Kuna umhimu wa kupata Katiba mpya, na kama tunataka katiba mpya tuzingatie maoni ya msingi, ila ukisikiliza maoni ya viongozi wanaotaka katiba mpya wanataja madaraka tu, langu kubwa tu zingatie maoni ya wananchi kwenye sekta zote nne walizozitaja.” Amesema Jaji Warioba.