Waziri Lugola Afanya Ziara ya Vituo vya Polisi vya Tabata, Buguruni Atoa Maagizo Mazito

Waziri Lugola Afanya Ziara ya Vituo vya Polisi vya Tabata, Buguruni Atoa Maagizo MazitoWAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amefanya ziara ya kushtukiza kituo cha Polisi Tabata na Buguruni vya jijini Dar es Salaam ili kujua kama maagizo yake aliyoyatoa katika vituo mbalimbali kama yameanza kufanyiwa kazi.



Waziri Lugola alianza ziara yake saa 2:45 jana asubuhi kwa kuibukia katika kituo cha Tabata na moja kwa moja alianza kuulizia mahudhurio ya wafanyakazi wote wa kituo hicho na kujua nani yupo kazini na nani hayupo na kwanini hajafika ofisini hapo kwa muda huo wa asubuhi.



Wakati alipokua kituoni hapo, pia Lugola alikichukua kitabu cha taarifa za watuhumiwa wote waliopo mahabusu na baadaye kuelekea katika mahabusu hiyo akiwahoji watuhumiwa kwa kuwaita kwa majina kujua makosa yao yaliyoyafanya wawepo kituoni hapo.



Lugola baada ya kumaliza katika kituo hicho, saa 5:27 alielekea kimyakimya katika kituo cha Polisi cha Buguruni, na aliwahoji watuhumiwa waliopo mahabusu katika kituo hicho na kujua makosa mbalimbali yanayowakabili huku polisi wapepelezi wa tuhuma zao wakiwepo katika tukio hilo.



Akizungumza mara baada ya kumaliza ziara yake, Lugola alisema, alitoa maagizo mbalimbali katika ziara zake nchini, hivyo anafuatilia kujua maagizo yake yameanza kufanyiwa kazi au bado baadhi ya vituo kama wameyapuuza.



“Lengo la hii ziara yangu ni kuboresha utendaji kazi wa vituo vya polisi nchini, sijaja kumuadhibu mtu mimi, hivyo msiwe na wasiwasi, bali kilichonifanya hapa nije nikufuatilia maagizo mbalimbali ambayo niliyatoa kama kweli mnayafanyia kazi,” alisema Lugola.



Maagizo aliyoyatoa mwezi miwili iliyopita katika ziara zake mikoa mbalimbali nchini ni kuhakikisha pikipiki zinaondolewa katika vituo vya polisi, dhamana zitolewe saa 24 ikiwemo Jumamosi na Jumapili, pamoja na polisi kutowabambikizia kesi wananchi.



Hata hivyo, Lugola alivipongeza vituo hivyo vya polisi vilivyopo wilayani Ilala na pia Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma alichokitembelea wiki iliyopita, kwa kuanza kuyafanyia kazi maagizo yake aliyoyatoa zikiwemo baadhi ya bodaboda, zimeondolewa vituoni na zilizobaki zina kesi mahakamani.



“Nilifanya ziara ya kushtukiza pale Kituo cha Polisi cha Tabata, na pia nimekuja hapa Buguruni, kwakweli wameaanza kuyafanyia kazi maagizo yangu, pikipiki zote nilizozikuta zinasababu yakuwepo hapo, na si vinginevyo kama walivyokua wanaziweka kiholela hapo awali,” alisema Lugola.



Pia lugola aliwataka Makamanda wa polisi nchini kuwafuatilia askari wao kwa umakini ili kujua utendaji kazi wao, na pia Waziri huyo alisema atakua anafanya ziara kama hizo mara kwa mara hivyo vituo vya polisi nchini viwe sawa muda wote.



“Hamjui siku wala saa ambapo nitakuja, tufanye kazi, tuwahudumie wananchi, tusiwaonee wananchi, tujitume kufanya kazi kwa weledi, sitamvumilia mtu ambaye atavunja utaratibu,” alisema Lugol
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad