Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema baadhi ya askari ndani ya Jeshi la Polisi bado wanaendekeza vitendo vya rushwa na kuwaambia dawa yao iko jikoni.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Namibu, Jimbo la Mwibara juzi, Lugola alisema baadhi ya polisi wanalichafua jeshi hilo kutokana na tamaa zao, hivyo kusisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano si ya kuchezewa.
Alisema licha ya kutoa taarifa mara kwa mara kuwataka askari hao kufanya kazi kiuadilifu kwa kuacha tabia ya kuomba rushwa, baadhi yao hawajamwelewa, hivyo kuahidi kupambana nao mpaka jeshi hilo litakapokuwa safi.
Lugola alisema anapokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi kuwalalamikia baadhi ya polisi kufanya matukio hayo ambayo hayakubaliki. Aliwataka askari hao wajue kuwa kati ya maagizo aliyopewa na Rais John Magufuli ni kupambana na rushwa ndani ya wizara hiyo, hivyo hawezi kumwangusha.
“Jeshi la Polisi linalinda usalama wa raia na mali zao, linapambana na rushwa katika mambo mbalimbali yakiwamo ya ardhi hapa kijijini, hivyo ndugu wananchi mnapopata migogoro mbalimbali ikiwamo ya ardhi na mengineyo, hakikisheni mnatoa taarifa polisi ili kusaidiwa,” alisema Lugola.
Alisema anapofanya ziara sehemu mbalimbali nchini anapokea maswali na pia anatumiwa ujumbe wa maandishi kwa njia ya simu kulalamikia tabia ya baadhi ya askari polisi ambao wanaomba rushwa hasa wale wa usalama barabarani.
Lugola aliongeza kuwa licha ya kuwa polisi wanaendelea kupambana na rushwa, nchi iko salama, hivyo wananchi popote wanapaswa kuwa na amani na kuendelea kufanya shughuli za maendeleo.
“Mimi sitakubali kuona mwananchi anateseka, mwananchi anaonewa, nasema hivi hao askari ambao ni wachache sana nitahakikisha ninapambana nao bila huruma. Kwa nini mnaonea wananchi ambao wengi wao ni maskini kwa kuwaomba rushwa. Hii haijakaa sawa,” alisema Lugola.
Lugola ambaye Septemba mwaka huu, alitangaza kuwa vituo vya polisi vifanye kazi saa 24 kwa kutoa dhamana kwa mwananchi yeyote mwenye sifa bila kujali ni Jumamosi au Jumapili, akiwa na maana kuwa ataondoa rushwa katika vituo, pia alitangaza kupambana na askari wala rushwa na watumishi wote walioko wizarani kwake na serikali kwa ujumla.