Zitto na wenzake waomba zuio la Mahakama bungeni

Zitto na wenzake waomba zuio la Mahakama bungeni
Wakili anayewakilisha wanasiasa wa upinzani wanaopinga Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Mpare Mpoki ameiomba Mahakama kuweka zuio kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bunge na Kamati zote zinazohusiana na muswada huo kutokuujadili wala kuuwasilisha bungeni hadi shauri lao litakapoamriwa.


Mpoki ametoa ombi hilo leo Mahakama kuu ambapo amesema kuwa Kamati za Bunge zinatarajiwa kuanza Januari 15, 2019 hivyo iwapo mahakama haitapanga muda mfupi shauri lao litakuwa limepitwa na wakati kwa kuwa litakuwa limeshashughulikiwa na Bunge.

“Hivyo kwa unyenyekevu tunaiomba mahakama hii itoe zuio la muda dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali asiwasilishe tena bungeni muswada huu kwani vinginevyo waombaji wataathirika kwa kiwango ambacho hawawezi kufidiwa,” amesema Mpoki.

Hata hivyo ombi la Mpoki limepingwa na Mwanasheria wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo ambaye amesema kanuni za  kuwekewa zuio la muda dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mamlaka nyinginezo za Serikali ikiwemo kamati ya Bunge, kutojadili muswada huo hazijakidhi kanuni za zuio la muda.

Jopo la majaji watatu wanaosikiliza shauri hilo wakiongozwa na Jaji Barke Sahel wameahirisha shauri hilo kwa muda hadi saa nane mchana leo Ijumaa Januari 4, 2019 kwa ajili ua uamuzi.

Kesi hiyo ya kupinga muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa imefunguliwa na Kiongozi wa Chama cha ACTWazalendo, Zitto Kabwe na wenzake Joram Bashange na Salim Biman wote wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa niaba ya muungano wa wanachama wa vyama 10 vya upinzani, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad