Waziri Lukuvi agundua ujanja ukwepaji kodi wa ardhi

Waziri Lukuvi agundua ujanja ukwepaji kodi wa ardhi
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amegundua ujanja unaofanywa na baadhi ya wananchi wa Moshi mkoani Kilimanjaro kutochukua hatimiliki za ardhi kwa lengo la kukwepa kulipa kodi.

Kutokana na ujanja huo, Lukuvi ameagiza takribani hati 5,000 ambazo hazijachukuliwa katika wilaya hiyo, kuchukuliwa haraka na wahusika na watakaoshindwa kufanya hivyo watafikishwa mahakamani kwa kukwepa kulipa kodi.

Katika Manispaa ya Moshi, jumla ya viwanja 15,000 vimepimwa na kati ya hivyo ni hati 10,168 tu ndizo wamiliki wake wamejitokeza kuzichukua.

Aidha, Waziri Lukuvi alimwagiza Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi katika Wilaya ya Moshi kuhakikisha ifikapo Februari, mwakani anasitisha kesi za migogoro ya ardhi na kuanza kujikita katika kusikiliza kesi za wamiliki wa ardhi wasiolipa kodi ya ardhi, ili kuiwezesha serikali kukusanya mapato.

“Wote wasiolipa kodi iwe waliokuwa na hati au wasio na hati, lakini wanaishi katika maeneo ya mijini yaliyopangwa, ikifika Februari 2019 watafikishwa mahakamani na tutahakikisha wanadaiwa kuanzia kipindi walichomilikishwa na wakishindwa nyumba zao zitapigwa mnada,” alisema jana alipozungunza na zaidi ya wananchi 150 wa wilaya hiyo zaidi ya 150 waliojitokeza kuwasilisha kero zao.

Lukuvi katika programu maalumu ya Funguka kwa Waziri, alisema katika ziara yake wilayani Moshi amebaini kuna hati 5,000, huku baadhi zikiwa na zaidi ya miaka 18 hazijachukuliwa na wahusika.

Alisema ulipaji kodi ya ardhi si hiari na mtu yoyote anayeishi katika eneo la mjini aelewe kuwa anaishi kwenye eneo lililopangwa na lazima aishi kwa masharti ya mipango miji ya mamlaka husika. Alisisitiza kuwa mtu huyo lazima awe na hati na namna yoyote ya kukwepa kulipa kodi ni sawa na kosa la uhujumu uchumi.

Lukuvi alizitaka mamlaka za serikali za mitaa katika miji kuhakikisha wananchi wanaishi kwa sheria za mipango miji na kuepuka kuishi wanavyotaka, huku akiwataka kuacha kuishi kwa mazoea.

Katika hatua nyingine, Lukuvi alishangazwa na baadhi ya watendaji wa ardhi katika Wilaya ya Moshi kwa kushindwa kushughulikia kero za wananchi kwa wakati jambo alilolieleza kuwa linasababisha wananchi kushindwa kupatiwa hati kwa wakati, huku baadhi ya watendaji wakishindwa kujibu hata barua ambazo baadhi ni za tangu miaka ya 1990.

Wananchi wengi waliojitokeza kuwasilisha kero zao katika mkutano na Waziri Lukuvi, walilalamikia kuchukuliwa maeneo yao, huku mamlaka husika zikishindwa kuwatatulia kero zao kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa, hivyo kuwasilisha malalamiko yao kwa waziri mwenye dhamana ya ardhi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad