Waziri Mkuu Aagiza Uchunguzi Fedha Za Ukarabati Wa Hospitali
0
November 18, 2018
* Ni sh. milioni 700 zilitolewa Julai mwaka huu, hadi sasa hakuna kilichofanyika
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi aunde timu ya wataalamu kufuatilia sh. milioni 700 zilizotolewa na Serikali ili kukarabati hospitali ya wilaya ya Nachingwea ambazo hadi sasa hazijatumika.
Kadhalika, Waziri Mkuu timu hiyo ikague matumizi ya sh. milioni 400 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi kituo cha afya cha kata ya Kilimarondo zimeisha na ujenzi haujakamilika.
Alitoa maagizo hayo jana (Jumamosi, Novemba 17, 2018) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Kilimarondo, Nachingwea mkoani Lindi, baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya.
“Serikali haitaki mzaha na fedha za umma, hivyo Mkuu wa Mkoa unda timu ya wataalamu kutoka mkoani waje Nachingwea kufuatilia ni kwa nini fedha zimetolewa tangu Julai ili kukarabati hospitali ya wilaya ziwe hazijatumika hadi leo. Pia tujue kama kweli bado zipo.”
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya mbunge wa jimbo la Nachingwea, Hassan Masala kumueleza kwamba hadi sasa sh. milioni 700 zilizotolewa na Serikali mwezi Julai mwaka huu kwa ajili ya ukarabati wa hospitali ya wilaya bado hazijatumika.
Mbali na fedha hizo, pia mbunge huyo ameomba uchunguzi maalumu ufanyike kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Kilimarondo baada ya fedha zilizotolewa kumalizika na mradi badi haujakamilika.
Mradi huo wa ujenzi wa kituo cha afya ulitengewa sh. milioni 400 ambazo zimekwisha na zinahitajika sh. milioni 51 kwa ajili ya kumalizia, ambapo Waziri Mkuu ameagiza Halmashauri ihakikishe fedha hizo zinatolewa ili kukamilisha mradi huo.
Kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho cha afya kitakachokuwa kinatoa huduma mbalimbali zikiwemo za mama na mtoto na upasuaji kutawapunguzia wananchi kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 90 kutoka Kilimarondo hadi Nachingwea kufuata huduma za afya.
Kuhusu suala la upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme, Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kusambaza umeme katika maeneo yote ambavyo bado hayajaunganishiwa nishati hiyo nchini yataunganishiwa, ikiwemo na tarafa ya Kilimarondo.
Waziri Mkuu alisema Rais Dkt. John Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu, Serikali imetenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika maeneo yote kwa gharama ya sh. 27,000 tu.
Pia Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kwamba hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, NOVEMBA 18, 2018.
Tags