Tawi la Yanga la Manzese la jijini Dar es Salaam limeibuka na kutoa tamko lao kuwa, wao wanafahamu Yusuf Manji bado ni mwenyekiti wao huku likilitaka Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lisiwaingilie kwenye uchaguzi.
Kauli hiyo, wameitoa ikiwa ni siku moja tangu TFF itangaze tarehe ya uchaguzi ya Yanga ambayo ni Januari 13, 2019 kwa ajili ya kujaza baadhi za nafasi za wajumbe na mwenyekiti.
Kwa mujibu wa Championi Jumatano, katibu mkuu wa tawi hilo, Shabani Omary, alisema wao wanashangaa kuona BMT na TFF wakiwaingilia masuala mbalimbali likiwemo la kutamka hawamtambui Manji.
Omary alisema, Manji bado anafanya kazi za klabu kama kawaida na hilo limethibitishwa na viongozi wao, hivyo hawataki kuingiliwa katika hilo huku wakiwaomba wanachama wa klabu hiyo kutojitokeza TFF kwenda kuchukua fomu za kugombea.
“Ujue tunashindwa kuelewa, kama unakumbuka hivi karibuni TFF ilisema kuwa inamtambua Manji ndiyo mwenyekiti wetu na ndiyo sababu ya kumuondoa aliyekuwa ana kaimu nafasi ya Manji baada ya kuandika barua ya kujiuzulu katika nafasi hiyo kabla ya Sanga (Clement) kuondolewa.
“Kingine katika mkutano mkuu wa Yanga uliohudhuriwa na Waziri Mwakyembe (Harrison), wote kwa pamoja wanachama tuligomea barua ya Manji aliyoiandika kwa viongozi wa Yanga tukitaka kuendelea na Manji, hivyo tunashangaa kuwaona BMT na TFF wakiingilia mambo yetu wakisema hawamuoni akifanya kazi.
“Sasa hao BMT na TFF wanataka kumuona Manji akifanya kazi huko kwao? Sisi tunajua Manji anafanya kazi na Yanga na mara kadhaa amekuwa akikutana na viongozi akina Kaya (Omary) ambaye ni kaimu katibu, tunawaomba watuachie Yanga na Manji wetu, basi kama ni uchaguzi, uitishwe mkutano wa dharura kwanza,” alisema Omary.