Yusuf Manji Aitosa Rasmi Yanga

Yusuf Manji Aitosa Rasmi Yanga
Hatimaye kilichomfanya mfanyabiashara bilionea, Yusuph Manji, kukataa kurejea kwenye nafasi yake ya Uenyekiti wa Yanga, pamoja na kuombwa na watu mbalimbali, kimebainika.

Bilionea huyo ambaye alikuwa mstari wa mbele kusaidia na kuwapa raha mashabiki wa klabu hiyo ya Jangwani, amekataa rasmi kurejea kwenye nafasi yake na sasa wanajiandaa kwa uchaguzi wa kujaza nafasi zilizoachwa wazi.

Moja ya nafasi hizo ambazo Yanga wanatakiwa kuzijaza, ni ya mwenyekiti iliyokuwa ikishikiliwa na Manji baada ya juhudi za kumshawishi arejee kushindikana.

Baada ya wadau wa Yanga na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, kuingilia kati na kusimamia msimamo wake wa kukaa pembeni na timu hiyo, juzi Baraza la Michezo Tanzania (BMT), wametaka miamba hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara kufanya uchaguzi mkuu.

Taarifa za uhakika kutoka kwa mtu wa karibu na Manji zinadai kuwa, bilionea huyo amezuiwa na familia yake hasa mkewe kuendelea na masuala ya soka na kumtaka atulize akili yake baada ya kupitia kwenye changamoto nyingi.

Taarifa hizo zinadai kuwa familia imemwambia wakati alipokuwa kwenye matatizo, baadhi ya watu wa Yanga hawakuonyesha kumjali huku wengine wakimwombea azidi kupatwa na mabaya ndiyo maana wamemshauri kupumzika.

“Kuna wengine walifikia hatua walitaka afungwe ili wafanye mambo yao, walimchukia kupita kiasi kisa kuifadhili timu,” kilisema chanzo hicho cha ndani.

“Japo aliweza kutoa fedha zake bila kinyongo lakini kuna watu walikuwa wanaona kama anafaidika Yanga, huku wakitamani siku yoyote aondoke waingie wao,” kiliongeza chanzo hicho.

Alisema pia kuna baadhi walitamka hadharani kuwa Yanga inaweza kujiendesha yenyewe bila Manji, kwani ina matajiri kibao wanaohitaji nembo ya klabu hiyo.

“Mwacheni apumzike, biashara zake nyingi zimeyumba, hao wanaojifanya wanajua sasa ni wakati wao wa kuvaa viatu vyake kipindi hiki akitafakari, ’’ alisisitiza.

“Anaipenda sana timu lakini kwa hali ilivyokuwa anahitaji kupumzika, labda kwa siku zijazo huko mbeleni anaweza kuja kivingine ila kwa sasa hivi hiyo ndio hali halisi amezuiwa,’’ kilimaliza chanzo hicho.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad