MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji atarejea klabuni hapo muda wowote kuanzia sasa lakini sura ya kwanza atakayoitambulisha kwenye uongozi wake ni mwanamichezo msomi, Ally Mayay Tembele.
Lakini Mayay mwenyewe ambaye inadaiwa anapigiwa chapuo kuwa Makamu wa Manji kwenye uchaguzi huo ujao, aliliambia Championi jana Jumanne kwamba hana taarifa yoyote kuhusu hilo. Manji ametoa masharti hayo ikiwa ni siku chache tu baada ya Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na michezo DK.
Harrison Mwakyembe, kumaliza utata uliokuwa umeibuka juu ya muundo wa uchaguzi wa klabu hiyo kwa kuwataka wanachama wahakikishe wanaingia kwenye uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi.
Kiongozi huyo inadaiwa amekubali kurejea kuendelea kuiongoza timu hiyo lakini ametoa sharti moja la kutaka kufanya kazi ndani ya timu hiyo akiwa na kigogo wa kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara mwenye Shahada ya pili ya juu ya masuala ya utawala wa biashara.
Kikikuzungumza na Championi Jumatano, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga, kimeeleza kuwa licha ya kamati ya uchaguzi kupitisha maazimio ya uchaguzi huo lakini mwenyekiti ametoa mapendekezo yake ya kufanya kazi na kigogo huyo kwa kuwa anaamini ataisaidia Yanga kufika mbali.
“Ni kweli mwenyekiti amekubali kurejea lakini ameomba pengine hadi wakati wa dirisha dogo la usajili litakapokuwa limefunguliwa kwa sababu kuna baadhi ya mambo yake anamalizia kuweka sawa na ikizingatiwa tayari wazee wa klabu wameridhia kurejea kwake.
“Sisi cha msingi kwetu ni kuendelea kuomba dua ili mipango iweze kuwa sawa ingawa ametoa mapendekezo yake ya mmoja kati ya watu anaotaka kufanya nao kazi kwenye safu yake ya uongozi ni Ally Mayay kwa sababu ya uelewa wake na mapenzi yake kwa timu yetu.
“Unajua Mayay amecheza Yanga kwa mafanikio makubwa na anaifahamu vizuri timu na mwenyekiti anaona uwepo wake utasaidia mambo mengi ukizingatia bado ana elimu kubwa ya mambo ya biashara kwake anaona itakua msaada ndiyo maana amempendekeza,” kilisema chanzo hicho.
Mayay alipoulizwa jana alisema kama kweli itakuwa hivyo yuko tayari kufanya kazi na Yanga lakini anaamini kwamba Manji ni muumini wa demokrasia na ataacha wanachama wafanye maamuzi.
Mchezaji huyo aliichezea Yanga kwa mafanikio mwanzoni mwa miaka ya 2000 kabla ya kutundika daruga kutokana na majeraha ya mara kwa mara na kuamua kurejea darasani kama alivyofanya pia straika matata wa enzi hizo, Aaron Nyanda.