Watu zaidi ya 80, wengi wao wakiwa wanafunzi, wametekwa nyara katika shule moja ya bweni magharibi mwa Cameroon.
Wanafunzi 79 pamoja na watu wengine watatu akiwamo Mwalimu Mkuu wa shule hiyo walichukuliwa msobemsobe na watu wenye silaha mapema asubuhi siku ya Jumatatu, Novemba 6 katika jiji la Bamenda.
Kiongozi mmoja wa serikali ameimbia BBC kuwa operesheni kali ya kuwakomboa mateka hao inaongozwa na jeshi na wanaimani kuwa watapatikana .
Majimbo ya Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi ya Cameroon yamekumbwa na uasi wa makundi ya wanaotaka kujitenga na nchi hiyo.
Gavana wa jimbo la Kaskazini Magharibi Adolphe Lele L'Afrique amevishutumu vikundi vya waasi kwa tukio hilo la utekaji.
Makundi ya wanamgambo ambao wanataka uhuru wa mikoa inayoongea Kingereza wanahamasisha watu kutopeleka watoto shule.
Lakini mpaka sasa hakuna kundi lolote ambalo limejitokeza na kukiri kutekeleza shambulio hilo katika Shule ya Sekondari ya Presbyterian Secondary ambayo ina wanafunzi wenye umri kati ya miaka 10 na14.
Video ya baadhi ya watoto hao, ambayo inaaminika kuchukuliwa na mmoja wa watekaji, imesambaa katika mitandao ya kijamii.
Wanafunzi hao, ambao wote ni wavulana, wamejazwa ndani ya chumba kimoja kidogo wanaonekana wakiwa wamejawa na woga wakati mtu aliyeshika kamera akiwaamuru wataje majina yao na wapi wanapotokea.
Wote wanarudia kauli moja: "Nilichukuliwa shule jana usiku na Amba boys. Sijui nipo wapi."
Amba ni kifupisho cha Ambazonia, ambalo ni jina la nchi ambayo waasi wanataka kuianzisha.
Mwanafunzi mmoja ambaye alifanikiwa kujinasua katika mkasa huo kwa kujificha chini ya kitanda ameiambia BBC kuwa kila kitu kilitokea kwa haraka baada ya watekaji kuingia shuleni hapo.
"Walimpiga rafiki yangu bila huruma. Kitu pekee ambacho nilikuwa nikifikiria ni kukaa kimya. Walitishia kuwapiga risasi baadhi ya watu...walikamata wavulana wakubwa wote na kuwaachia wadogo."
Kiongozi wa Kanisa la Presbyterian nchini Cameroon, Mchungaji Fonki Samuel Forba ameiambia BBC kuwa tayari ameshaongea na watekaji.
"Hawataki pesa yoyote ya komboleo. Kitu pekee wanachotaka ni sisi kufunga shule zetu.Tumewaahidi kuwa tutazifunga," mchungaji Forba ameiambia BBC.
"Tunatumaini na kusali kuwa watawaachia wanafunzi na walimu," ameongeza.
Hii si mara ya kwanza kwa wanafunzi kutekwa nyara katika eneo hilo, anaripoti mwandishi wa BBC Ngala Killian Chimtom.
Oktoba 19, wanafunzi watano kutokA Shule ya Sekondari ya Atiela walitekwa na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha. Mpaka sasa bado haijulikani walipo.
Waasi wanadai kuwa mfumo wa elimu wa Cameroon unakandamiza mfumo wa wale wanaozungumza Kingereza katika majimbo hayo mawili.
Wanamgambo wanaonaka kuanzisha walianza kuibukia mwaka 2017 baada ya vikosi ya usalama kutumia nguvu kuzima maandamano ya watu wengi.
Maandamano hayo yalikuwa yanaongozwa na wanasheria na walimu wakipinga kile walichodai ni kushindwa kwa serikali ya Yaoundé kipa thamani inayotakiwa mifumo ya elimu na kisheria ya Kingereza katika majimbo hayo mawili.
Serikali ambayo inaongozwa na Rais Paul Biya toka mwaka 1982 imekuwa ikishutumiwa vikali kwa kutegemea watumishi wanaotokana na mfumo wa Kifaransa kuendesha shughuli za umma katika majimbo hayo hali ambayo inawakandamiza wale wanaozungumza Kingereza ambao ni wastani wa 20% ya raia wote wa nchi hiyo.