Alichokisema Rais Magufuli Baada ya Kutia Saini ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge
0
December 12, 2018
Rais John Magufuli ameshuhudia utiaji saini wa ujenzi wa mradi wa umeme wa Bonde la Mto Rufiji wa Stiegler’s Gorge kati ya Serikali ya Tanzania na Misri, akibainisha kuwa mradi huo utasaidia kutunza mazingira tofauti na baadhi ya wanamazingira wanavyokosoa.
Akizungumza leo Jumatano Desemba 12, 2018 Ikulu Dar es Salaam katika utiaji saini huo ulishuhudiwa pia na Waziri Mkuu wa Misri, Mostafa Madbouly, Magufuli amesema mradi ulipigwa vita kwa kisingizio cha kulinda mazingira na kusisitiza kuwa unalenga kutunza hayo mazingira.
"Lazima tujifunze kwa waliotutangulia, sisi tuna megawati 1500 wenzetu wa Misri wana megawati zaidi ya 25,000 na maji wanayotumia yanatoka Kagera, lakini kwetu hata hapo Kagera umeme hakuna.
"Nawaomba watanzania hasa wale wanaopenda kusemasema wasitumiwe na mabeberu, huu mradi hauna dini, si wa chama, huu ni mradi wa watanzania wote na ni kwa faida yetu sote watanzania, naomba wasitumiwe na mabeberu.
"Nawapongeza watanzania kwa kutekeleza mradi huu, ndio maana nasisitiza tulipe kodi. Kuamua ni kitu kigumu, nashukuru wabunge na watanzania kwa kuamua, tungeanza hata kutekeleza kidogo kidogo leo tusingefikia hapa au a kupata matatizo haya ya umeme.
"Mradi huu una baraka nyingi, nimekaa kwenye wizara ya ujenzi kwa miaka 23 na tulisaini miradi mingi lakini sijawahi kuona mradi ambao wakati wa utiaji saini kuwa na idadi ya viongozi wetu wa dini kiasi hiki, ndio maana nasema mradi huu umebarikiwa.
"Tulipoomba watukopeshe kwa ajili ya mradi huu wakakataa lakini tulipowaambia kuhusu kuingia ubia wakakubali, maana yake ubia ni biashara na wao ndio watatupangia bei, ukiona nchi imefikia hatua ya kupangiwa bei ujue tumekwisha, ipo siku watasema hatuwashi kabisa.
"Wakati tunakaribia kutia saini mkataba huu, Mhe. Rais wa Misri niliongea nae alisema atashindwa kuhudhuria tukio hili lakini ameniambia mradi huu ataubeba kama mradi wake.
"Tukikamilisha mradi huu, umeme utapatikana kwa bei rahisi, hata bidhaa za viwanda zitauzwa kwa bei ya chini, uchumi wa nchi utakua lakini pia uchumi wa mwananchi mmoja mmoja utakua.
"Wapo wanaosema kuwa mradi huu utaharibu mazingira, si kweli hata kidogo, Mradi huu ni rafiki wa mazingira kwasababu umeme wa maji ni rafiki wa mazingira, lakini eneo litakalotumika ni 1.8% hadi 2%.
"Mradi huu tuliona unafaa kwa sababu chanzo chake ni cha uhakika, gharama zake si kubwa kulinganisha miradi ya vyanzo vingine, lakini pia mito yake ni kutoka sehemu ambazo hupata kiasi kikubwa cha mvua kwa mwaka.
"Nimefurahi baada ya miaka 40 mradi huu unatakelezwa, ni furahi zaidi unatekelezwa kwa fedha zetu wenyewe, utagharimu shilingi trilioni 6.558, wakati Yesu anawakimbia watesi wake alikimbilia nchi ya Misri, na sisi pia kwenye swala la umeme tumekimbilia Misri."Amesema Rais Magufuli
Tags