Anayetuhumiwa Kumhonga Waziri Lukuvi Akutwa na Kesi ya Kujibu

Anayetuhumiwa Kumhonga Waziri Lukuvi Akutwa na Kesi ya Kujibu
Mfanyabiashara Mohamed Kiluwa (50) amekutwa na kesi ya kujibu katika mahakama ya Wilaya ya Ilala na ataanza kujitetea Desemba 17, 2018.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne Desemba 11, 2018 na hakimu mkazi, Samuel Obasi  baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.

Kiluwa anakabiliwa na shtaka moja la  kutoa rushwa ya Dola za kimarekani 40,000 kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  William Lukuvi.

Akisoma Uamuzi huo baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao leo,  Hakimu Obasi amesema "Upande wa mashtaka ulileta mashahidi sita pamoja na vielelezo vingi ikiwemo hati za Ardhi na CD.”

Hakimu Obasi amesema amepitia ushahidi wa mashahidi hao pamoja na vielelezo na kumuona  mshtakiwa kuwa ana kesi ya kujibu.

“Baada ya kupitia ushahidi na vielelezo hivi, mahakama yangu imemkuta Kiluwa ana kesi ya kujibu, hivyo chini ya kifungu namba 231(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, mshtakiwa anatakiwa kujitetea,” amesema Obasi.

Baada ya kueleza hayo wakili wa mshtakiwa, Omary Madega amedai upande wa utetezi watakuwa  na mashahidi wawili, akiwemo Kiluwa.

Awali, kabla ya hakimu kutoa uamuzi huo  upande wa mashtaka walikuwa na shahidi moja ambaye alitoa ushahidi wake dhidi ya Kiluwa.

Shahidi huyo,  Wilson Luge (39) ambaye ni Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Wizara ya Ardhi, amedai kuwa yeye ndio aliyeshiriki zoezi la kuhakiki na kuhesabu fedha hizo Dola za 40,000 za Marekani ambazo zilikuwa katika bahasha ya kaki, juu ya meza ya waziri Lukuvi.

Akiongozwa na mawakili kutoka Takukuru, Maghela Ndimbo akisaidiana na Nikson Shayo, Luge ambaye ni shahidi wa sita katika kesi hiyo, amedai kuwa baada ya kuzihesabu fedha hizo walizianisha katika fomu maalum na kisha kuisaini fomu hiyo kama sheria inavyotaka.

Hakimu Obasi ameahirisha kesi hiyo hadi  Desemba 17,2018 itakapoendelea kwa upande wa utetezi kuanza kujitetea.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad