Askofu Ataja Dawa ya Watoto wa Mitaani

Askofu Ataja Dawa ya Watoto wa Mitaani
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa, amewataka Wakristo kuitumia sikukuu ya Noeli kuimarisha upendo wa familia, akiamini ni dawa dhidi ya changamoto ya watoto wa mitaani.

Askofu Ngalalekumtwa alitoa ujumbe huo wakati wa misa ya mkesha wa sikukuu ya Krismasi iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu Kihesa mjini Iringa.

Alisema ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi linatokana na kutoweka kwa upendo katika familia, hali inayosababisha wazazi hasa wanaume kutelekeza familia zao, huku baadhi ya watoto nao wakizikimbia familia na kwenda kuishi kwenye mazingira hatarishi.

Aliwataka waumini wa kanisa hilo kuwa kielelezo cha Maria na Yosefu kwa kudumisha upendo katika ndoa zao na kutengeneza mazingira rafiki kwa malezi ya watoto wao.

"Tumeshuhudia wazazi wakitelekeza familia na kuwaacha watoto, hali hii inasababisha watoto kuishi katika mazingira hatarishi. Hali hii ni hatari kwa ustawi wa jamii na taifa letu kwa kuwa familia kama hiyo haiwezi kuzalisha viongozi bora wa baadaye," alisema.

Askofu Ngalalekumtwa aliongeza: "Tunapoadhimisha Noeli tunatakiwa kuwa na nia njema na mioyo iliyotakata kwa kuwasaidia wajane, yatima na wale wote wasiojiweza ili nao wajione kuwa ni Taifa la Mungu."

Askofu huyo pia aliwahimiza waumini wa kanisa hilo kuendelea kuiombea amani Tanzania ili tunu hiyo isitoweke na kusababisha nchi kuingia katika vurugu au machafuko ya namna yoyote.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad