MAMBO vipi mpenzi msomaji wa safu yako hii upendayo ya Staa na Familia? Ni matumaini yangu upo poa. Kama kawaida hapa tunawaletea mastaa mbalimbali wa Bongo na familia zao.
Wiki hii tunaye staa wa sinema za Kibongo, Aunt Ezekiel ambaye atatuelezea anaishije yeye na mtoto wake mmoja wa kike aitwaye Cookie;
Kwa nini aliamua kumpa mwanaye jina la Cookie?
“Unajua maana ya Cookie ni vibiskuti vile vidogo, lakini vitamu sana, sasa nilipomzaa tu niliona nimepata kitu kitamu sana kuliko chochote hapa duniani, nikaamua tu kumpa mtoto wangu jina hilo kumuonesha kwamba yeye kuwa mwanangu ni utamu tosha kwangu.
Alipanga kumzaa Cookie au iliyotokea tu?
“Niliamua kabisa kwa sababu mimi siyo mtoto mdogo hivyo kama nisingeitaka mimba, nisingeiacha ikue. Lakini kwa vile nilitamani sana mtoto, nilijipanga kumpokea kwa moyo wote.
Nini anachokipenda kwa mwanaye?
“Ni mtoto ambaye anajiamini sana, lakini kingine ana upendo mkubwa kwa kila mtu, yaani hana ubaguzi na ninafikiri hiyo ni kwa sababu ameishi na watu tofauti na ana busara zake, yaani hata kama uko kwenye wakati mgumu unakuwa sawa.
Alitamani Cookie afanane na yeye au baba yake?
“Kiukweli nilitamani afanane na baba yake hata kabla sijamzaa na Mungu akajalia hivyo sasa kuna wakati mwingine hata tukigombana na baba yake nikimuangalie yeye narudisha upendo tena kwa baba yake, nazidi kumpenda.
Ni kitu gani amekipanga mbeleni kuhusu mwanaye?
“Nimepanga aje kuwa msomi huko mbeleni na ndiyo maana nimetenga pesa zake nyingi tu za kumsomesha sasa hivi mpaka darasa la saba bila bugudha yoyote alafu nyingine ya kuendelea na masomo ndiyo nimeanza kuweka sasa.
Anapata muda wa kuwa na mtoto wake?
“Kwa nini nisipate muda wa kuwa na mwanangu? Ni kweli kuna muda nabanwa sana na kazi yangu, mara kukaa kambini na vitu vingine, lakini nikitulia nakuwa naye muda mrefu sana na kingine napenda sana kusafiri naye hivyo nakuwa na muda wa kutosha mno kuwa pamoja naye.
Ana mpango wa kuzaa mtoto mwingine?
“Natamani sana, lakini bado kidogo, kuna vitu navikamilisha alafu ndiyo nifikirie kuzaa mtoto mwingine, siyo mmoja hata watatu kwa sababu mimi napenda sana watoto.”