Bao la kwanza alilofunga mshambuliaji wa timu ya Coastal Union, Ally Kiba dhidi ya Mawezi jana katika uwanja wa Jamhuri Morogoro limewafurahisha mashabiki na kumtabiria makubwa kwenye kombe la shirikisho pamoja na Ligi Kuu.
Kiba alifunga bao hilo dakika ya 5 kwa mkwaju wa penati katika mchezo huo wa kirafiki ambao walishinda kwa jumla ya mabao 2-1 ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Tanzania Prisons, hali iliyoleta mjadala kwa mashabiki wa soka kwenye mitandao ya kijamii.
Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema mashabiki wamefurahi kuona Kiba akiwa uwanjani na ameweza kuonyesha uwezo wake alionao nje ya kazi ya muziki ambayo anaifanya.
"Kiba ana nafasi ya kufanya vizuri kwenye mpira kama ambavyo anafanya kwenye muziki, sababu kubwa ni usikivu alionao na wepesi wa kuweza kuelewa yale anayofundishwa, ni jambo la wakati kudhhihirisha haya ninayoongea," alisema.
Kiba amecheza michezo 2 Ligi Kuu ambapo mchezo wa kwanza alicheza dhidi ya Kagera Sugar kwa muda wa dakika 2 na ule dhidi ya Mbeya City ambao alicheza kwa muda wa dakika 64.