Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Kuendelea Kuyafunga Maduka ya Kubadilishia Fedha

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Kuendelea Kuyafunga Maduka ya Kubadilishia Fedha
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amesema wataendelea kudhibiti biashara ya ubadilishaji fedha ili kuhakikisha sekta ya fedha haiyumbi nchini.

Amesema BoT ina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni zinazoweza kutumika kwa kipindi cha miezi mitano.

Novemba mwaka huu, BoT ilifunga zaidi ya maduka 100 ya kubadilishia fedha mkoani Arusha yaliyoshindwa kukidhi masharti ikiwamo kutokuwa na leseni halali.

Akizungumzia suala hilo leo wakati wa kikao cha kazi kati ya Rais John Magufuli na Mamlaka ya Mapato (TRA) na wakuu wa mikoa, Profesa Luoga amesema BoT inachukua jitihada mbalimbali kuhakikisha sekta ya fedha inazidi kuimarika.

“Udhibiti utaendelea kuwa mkali. Hii ni moja ya hatua zitakazoendelea, kanuni ambazo zilikuwepo ziliongeza udanganyifu na maduka yakazidi kuongezeka kiholela,” amesema.

Amesema hakuna haja ya kuwa na maduka mengi ya kubadilishia fedha badala yake yatapatikana katika sehemu maalumu pekee ikiwamo hoteli za kitalii na benki.

“Hatuhitaji maduka 100 ya kubadilisha fedha Dar es Salaam, kwani kuna benki za kutosha. Tunahitaji maduka ya fedha kwenye sehemu muhimu kama kwenye mahoteli ya kitalii na mipakani,” amesema.

 Aidha, amewaonya wafanyabiashara wanaobeba fedha kwenye mabegi wanapoenda kulipia bidhaa nje ya nchi akisema kufanya hivyo ni kuvunja sheria.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad