Mbunge wa jimbo la Ubungo, Saed Kubenea (CHADEMA) amewataka wananchi wa Ubungo kuhifadhi vyema nyaraka zao za maeneo waliyobomolewa na kwamba CHADEMA ikiingia madarakani watahakikisha wanawalipa fidia zao.
Kubenea ameyasema hayo jana ikiwa ni siku moja kupita tangu Rais John Pombe Magufuli alipotamka hadharani kuwa wahanga waliobomolewa nyumba kuanzia maeneo ya Ubungo hawatalipwa fidia kwa kuwa walivunja sheria kwa kujenga kwenye hifadhi ya barabara.
Akizungumza jana na wanahabari, Kubenea amedai kushangazwa na kauli ya rais kwamba waliovunjiwa nyumba walijenga kwenye hifadhi ya barabara lakini serikali ndiyo iliyokuwa ikipokea kodi zao, kuwapatia hati za maeneo, kuwawekea maji na umeme huku wakijua hilo ni eneo la hifadhi.
"Naomba wananchi wa Ubungo, Kimara waliovunjiwa nyumba zao wahifadhi vizuri nyaraka zao. Mungu akipenda Sisi CHADEMA tukiingia madarakani tutalipa waathirika wote waliobomolewa kuanzia ubungo hadi Kibaha. Inawezekana siyo lazima CHADEMA waingie madarakani lakini anaweza akaja kiongozi mwingine akalipa. Hii inawezekana," alisema Kubenea.
Akiipigilia msumari kauli yake, Kubenea alisema kwamba, "Jumuiya ya Afrika Mashariki ilivunjika 1977, Serikali ya Mwl. Nyerere haikuipa kipaumbele kuwalipa wastaafu na hata seriakali ya Rais Mwinyi, ila serikali ya Mkapa yenyewe ililipa ikiwa ni baada ya miaka 30. Hivyo wanaweza wasipate wao malipo hayo lakini vizazi vyao vitakuja kunufaika ndiyo maana zipo nchi sasa zinalipwa fidia kutokana na vita vya dunia".