Siku chache baada ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kumuahidi Rais John Magufuli kuwa mwaka 2020 atamkabidhi mkoa ukiwa na viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi, Chadema imelaani kauli hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Desemba 24, 2018 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye amesema kauli hiyo ya Makonda inalenga kufuta vyama vya upinzani na kuiacha nchi ya chama kimoja.
“Ahadi yake kwa Rais inamaanisha ataendelea kuvunja Katiba kwa kukandamiza upinzani ikiwemo kutumia vyombo vya dola ili kutimiza malengo yake,” amesema.
Sumaye ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu amesema kwa mamlaka aliyonayo mkuu huyo wa mkoa hakupaswa kutoa kauli hiyo inayoonyesha wazi uvunjaji wa Katiba.
“Makonda amekuwa akifanya mambo mengi ya kuidhalilisha Serikali, kinachoonekana huenda kazi aliyopewa ni kubwa kuliko uwezo wake, aliyempa ambadilishie au yatakayofuata yatashangaza zaidi,” amesema Sumaye.