Kwamujibu wa maafisa wa serikali, harusi za kisasa si tu ni za gharama kubwa bali zinaenda kinyume na misingi ya kijamaa ya nchi hiyo.
Harusi za Kichina ambazo hufungwa kimila, hauambatana na sherehe ambazo kwa sasa mamlaka zinadai kuwa zimekuwa kubwa mno.
Sasa serikali ya Beijing inajipanga kuja na namna ya kuzifanya ziwe sawa kwa kufanyika kwa sherehe zenye kiasi.
Wachina kama ilivyo kwa raia wa nchi nyengine duniani wamekuwa wakishindana na jirani, marafiki na jamaa katika kuandaa sherehe kubwa na za kupendeza za harusi. Na harusi kubwa tayari zimeshakuwa fasheni nchini humo.
Harusi hizu huambatana na karamu kubwa, nguo za kifahari na safari za ughaibuni kupiga picha za harusi.
Pia, utaratibu wa asili wa kuwafanyia stihizai (mzaha) bibi na bwana harusi kabla ya ndoa - ili kuwaondolea woga katika siku yao kubwa- pia umetajwa kufanyika katika namna isiyokubalika katika siku za hivi karibuni.
Kumekuwa na ripoti kuwa wahudhuriaji harusi wamekuwa wakiwafania wanandoa vitendo vya stihizai vinavyodhalilisha na wakati mwengine hugeuka shambulio.
Wiki iliyopita bwana harusi mmoja aligongwa na gari wakati akikimbia utaratibu huo ambao alikuwa afungwe kamba na kupigwa.
Wiki mbili zilizopita, wapambe wa bibi harusi mmoja walijeruhiwa na vipande vya vioo baada ya wapambe wa bwana harusi kulazimisha kuingia katika nyumba yao kwa kuvunja mlango na shoka.
Wizara ya mambo ya kijamii ya nchi hiyo imelaani vikali matukio hayo "ya kifahari na upuuzi" na kutoa "mwongozo" wa kufanya harusi "ndogo na za na shrehe za kiasi", shirika la habari la Xinhua limeripoti.
"Sherehe zinapaswa kuzingatia misingi ya kijamaa na tamaduni za kichina ili kudhibiti mienendo hasi na kuwa mfano kwa jamii nzima. Mmamlaka zitatunga kanuni za mchakato wa harusi na ukomo wa zawadi na fedha," afisa wa wizara hiyo bw Yang Zongtao aliiambia runinga ya serikali Jumapili.
Hii si mara ya kwanza kwa China kujaribu kuwaelekeza wananchi wake namna ya kusherehekea ndoa zao.
Mwaka 2016,Chama cha Kikuministi kinachoongoza nchi hiyo rasimu ya mwongozo wa kusherehekea harusi kwa kuzingatia misingi ya chama hicho ya kubana matumizi yasiyo ya lazima.