
ITC ya Chirwa imetumwa kwa Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF) baada ya klabu yake ya zamani ya Nagoom FC ya nchini Misri kuthibitisha kuachana na mchezaji huyo ambayo sasa inampa uhuru wa kujiunga na timu yoyote.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Nurdin Amin ‘Popat’, amesema kwamba tayari kibali hicho kimeshatumwa TFF na sasa wanachosubiri ni kukamilika kwa vibali vyake vya kufanya kazi pamoja na leseni itakayomwezesha kucheza soka nchini Tanzania.
“Tunamshukuru Mungu leo jioni (jana) TFF imetupa taarifa ya kupokea ITC ya Chirwa kutoka Misri alipokuwa akicheza awali," amesema Abdulkarim Amim.
"Hataweza kuiwahi mechi ya leo kutokana na kutokuwa na leseni ya kucheza ligi na kibali chake cha kufanya kazi kutokamilika, tunatarajia atacheza mechi ijayo ya Ijumaa dhidi ya Mbao,” ameongeza.
Azam FC yenye alama 33, leo inashuka dimbani kucheza na Stand United katika uwanja wa Chamazi saa 1:00 usiku katika harakati ya kuendeleza rekodi yake nzuri ya kutopototeza mchezo wowote katika ligi kuu Tanzania bara msimu huu nyuma ya kinara Yanga.