KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Hassan Dilunga, ameweka rekodi ya kimataifa katika ardhi ya Bongo kutokana na kufanikiwa kuzivusha timu mbili kimataifa kwa nyakati tofauti.
Dilunga kwa sasa anaitumikia timu ya Simba lakini awali alikuwa mchezaji wa kutegemewa Mtibwa Sugar.
Rekodi ya kwanza aliyoiweka kwenye ardhi ya Bongo ni ile alipokuwa Mtibwa Sugar kwa kuisaidia timu yake kuweza kushiriki michuano ya kimataifa baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Singida United, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Rekodi ya pili baada ya kutua Simba msimu huu, akaipa Ngao ya Jamii baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar. Mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Jumapili iliyopita, Dilunga ameweka rekodi ya tatu nyingine ya kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Simba ambapo pasi yake ya mwisho ndiyo iliyozaa bao lililowapeleka kwenye hatua hiyo lililofungwa na Clatous Chama dakika ya 88.
Mara ya mwisho Simba kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ilikuwa mwaka 2003 baada ya kufanikiwa kuifunga Zamalek ya Misri kwa penalti 3-2.