Dk. Bashiru: Sitawavumilia Viongozi Wa CCM Wenye Uchu Wa Madaraka

 Dk. Bashiru: Sitawavumilia Viongozi Wa CCM Wenye Uchu Wa Madaraka
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Taifa, Dkt Bashiru Ally Kakurwa amewasisitiza wale wote wanaohitaji Uongozi katika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM, Kujipanga kwa Sifa, Sera nzuri zitakazowauza na si kwa kurubuni, wala kuhonga Wananchi.

Alisema hayo mwishoni mwa wiki mkoani Kagera, wakati akizungumza na viongozi wa Chama na Serikali pamoja na wananchi waliojitokeza kumpokea.

Katika maelezo yake, Dk. Bashiru amesisitiza juu ya wagombea kufanya siasa za maendeleo, na si siasa chafu za kugawa watu, kujikomba, kurubuni wala kutoa hongo huku akiwataka wanachama kuanza kubaini wanachama wenye sifa, wenye uchu na maendeleo  na wasioweka mbele masilahi binafsi, ili uchaguzi ujao uwe wa mfano, kama chaguzi zilizofanyika enzi za TANU.

Sambamba na hilo Dk. Bashiru amenukuliwa akisema, kiongozi atakaechaguliwa kwa kutumia njia za ulaghai hata kama atakuwa amepitishwa, akibainika ataenguliwa mara moja.

Katika hatua nyingine kiongozi huyo wa CCM amewataka viongozi waliopo madarakani waachwe wafanye kazi, kwani muda wa kuanza kunadi sera bado, hivyo kwa wale ambao wameaanza kupita pita kwa wanachama waache mara moja kwani tayari orodha yao anayo kwa nchi nzima.

Kuhusu wawekezaji, Dkt. Bashiru amesema Tanzania bado ni maskini na nyenzo pekee ya kujikwamua kutoka katika umasikini huo ni kupitia sekta ya kilimo, hivyo hapendezwi na hali iliyopo kwa sasa ya kuwaruhusu wawekezaji kutoka nje ya nchi kufanya shughuli za Kilimo, Ufugaji Na Uvuvi.

Hivyo, amemuagiza Naibu Waziri wa Kilimo, Innocenti Bashungwa kuwa kwa wale ambao wameshapewa nafasi ya Kufanya shughuli hizo wawe wa mwisho,  na kwamba ardhi ya Tanzania ilimwe na Watanzania wenyewe, na kuanzia sasa Wizara haitatakiwa kutoa vibali kwa wawekezaji katika Sekta ya Kilimo kufanya Kilimo ndani ya nchi yetu.

Dkt. Bashiru yupo Mkoani Kagera kwa Mapumziko mafupi pamoja na ziara ya kikazi aambapo kuanzia Disemba 26, mwaka huu ataanza ziara hiyo kwa kukutana na viongozi wa Chama kutoka Missenyi, Bukoba na Bukoba Mjini.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad