Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Ndani ametoa kauli hiyo leo Jumatano Desemba 26, 2018 wakati akizungumza na na gazeti la Mwananchi, kubainisha kuwa ana matumaini kuwa baada ya kumalizika kwa sikukuu ya Krismasi huenda mambo yakawa mazuri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema kesho atazungumza na waandishi wa habari ili kufafanua yote yanayoendelea baina ya mamlaka hiyo na Fastjet.
Katika maelezo yake Masha amesema Serikali haimpi ushirikiano wa kutosha katika mkakati wake wa kulifufua Shirika la Fastjet.
Amesema wamemzuia kuingiza ndege aina ya Boeing 737-500 baada ya iliyokuwepo kuzuiliwa kuruka kwa madai kuwa inapata hitilafu mara kwa mara na shirika halina meneja mwajibikaji.
Desemba 19, 2018 akizungumza katika kipindi cha 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds, Masha alisema ndege hiyo ingewasili Tanzania Jumamosi iliyopita Desemba 22, 2018 lakini hadi leo saa sita mchana ndege hiyo ilikuwa haijafika.
Leo amebainisha kuwa ikiwa ataruhusiwa ndege hiyo itafika Tanzania ndani ya muda mfupi kwa maelezo kuwa kila kitu kipo tayari, “safari kutoka Afrika Kusini ilipo hiyo ndege hadi Tanzania ni mwendo wa masaa matatu tu.”
Amesema ndege iliyozuiwa ilikuwa imelipiwa tayari kwa kuruka ikiwa na wafanyakazi wote, hivyo kitendo cha kuizuia ni hasara.
“TCAA inasema ili niweze kuingiza ndege hiyo nimalize kwanza madeni yote, baadhi ya madeni tayari yamelipwa na Fastjet Plc mengine Fastjet Tanzania,” amesema.
“Tayari tumemaliza lakini fedha imeisha, kwa kuwa tayari fedha nyingine tulizitumia kutimiza matakwa yao, wangeniruhusu nifanye kazi ili nipate fedha ya kulipa yaliyobaki.”
Credit:Mwananchi