HALI ya mambo ndani ya Yanga sasa si shwari tena kwani muda wowote kuanzia leo kipa namba moja wa timu hiyo, Beno Kakolanya anaweza kuvunja mkataba. Lakini yeye pamoja na Kevin Yondani wameshafungiwa.
Hali hiyo inatokana na uongozi wa Yanga kushindwa kufikia muafaka na kipa huyo juu ya madai yake ikiwa ni pamoja na malipo ya mshahara wake wa miezi minne.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni, Kakolanya pamoja na nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani, waligoma kujiunga na timu hiyo kwa ajili ya mechi za Kanda ya Ziwa dhidi ya Mwadui FC na Kagera Sugar, lakini pia baada ya timu kurudi Dar es Salaam, bado wachezaji hao wameendelea kuwa nje ya kikosi hicho wakitaka walipwe stahiki zao wanazodai.
Meneja wa Kakolanya, Selemani Haroub, alisema kuwa mpaka kufikia jana, kipa huyo na uongozi wa Yanga walikuwa bado hawajafikia muafaka juu ya jambo hilo kutokana na uongozi huo kutoonyesha ushirikiano.
“Tumekuwa tukiwatafuta viongozi wa Yanga na hasa katibu mkuu ili kuzungumzia suala hili lakini wamekuwa hawaonyeshi ushirikiano, kwa hiyo kesho (leo) ndiyo mwisho, baada ya hapo tutajua nini cha kufanya,” alisema Haroub.
Alipoulizwa Kakolanya kuhusiana na hilo, alisema: “Katika hili siwezi kusema lolote ila meneja wangu ndiye anayejua kuwa wamefikia wapi uongozi wangu. Ila ni kweli kuna mambo ambayo ndiyo yamesababisha nisiwe na timu mpaka sasa.”
Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya, alipotafutwa jana, alikuwa akikata simu mara kwa mara, huku Meneja wa Yanga, Nadir Haroub akisisitiza kuwa anachofahamu Beno bado ni mchezaji wa Yanga.
Katika hatua nyingine, kocha Mwinyi Zahera, amewafungia mechi mbili, Yondani na Kakolanya kutokana na kudaiwa kugomea kuichezea timu hiyo wakidai fedha za mshahara.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Championi Jumatatu, kwamba Zahera hana mpango kabisa wa kuwatumia wachezaji hao katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons (leo Jumatatu) sambamba na mchezo unaokuja dhidi ya Biashara United.
“Yeye kaona kwamba bora aendelee na wachezaji wachache ambao watakuwa na moyo wa kuitumikia timu tofauti na wale ambao wanagoma,” kilisema chanzo hicho.