Hii ndiyo Sababu ya Australia kumuomboleza kangaroo


Roger, kangaroo aliyejipatia umaarufu mkubwa kutokana na unene wake na misuli yake iliyotuna vilivyo ambayo angekuwa binadamu tungelisema alikuwa na 'six-pack', amefariki dunia akiwa na miaka 12. 

Wapenzi wa wanyama nchini humo wamekuwa wakiomboleza kifo chake. 

Kangaroo huyo aliokolewa angali mdogo kutoka porini baada ya mamake kuuawa katika ajali ya barabarani. 

Alikulia katika kituo cha kuwatuza kangaroo cha Kangaroo Sanctuary eneo la Alice Springs nchini Australia. 

Alinenepa haraka sana - na kufikia wakati wa kifo chake alikuwa na kimo cha 2m (6ft 5) na uzani wake ukawa 89kg. Akiwa amesimama, alikuwa mrefu kuliko binadamu wengi. 

Kituo hicho cha kuwatunza kangaroo kilisema mnyama huyo alifariki wikendi kutokana na 'uzee'. 
Walisema walikuwa wamempoteza "mvulana mtanashati". 

Chris "Brolga" Barns, anayesema alianzisha kituo hicho cha kuwahifadhi kangaroo kutokana na Roger na "wake zake kadha" anasema mnyama huyo alikuwa ndume mtawala katika kituo hicho kwa miaka mingi. 

"Alikuwa na kuwa kangaroo aliyependwa na watu kutoka kila pembe ya dunia, sawa na tulivyompenda sisi," alisema. 

Umaarufu wa Roger duniani ulianza mwaka 2015 baada ya picha zake akiiponda ponda ndoo ya maji iliyotengenezwa kwa chuma kwa mikono yake, huku misuli yake iliyotuna vilivyo ikionekana wazi. 

Katika uzee wake, alihangaishwa na ugonjwa wa yabisi kavu ambao huathiri mifupa na maungio na pia alianza kupofuka 

Lakini alikuwa anafurahia "maisha yake ya uzeeni", alisema Bw Barns mwaka 2016. 

Porini, kangaroo kwa kawaida huishi hadi miaka 10 hivi lakini wakiwa kwenye hifadhi wanaweza wakaishi miaka zaidi ya hiyo. 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad