Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, limetakiwa kufanya ukaguzi na uhakiki wa vibali kwa wamiliki wa silaha ili kudhibiti vitendo vya uhalifu, vinavyotokana na matumizi mabaya ya silaha hizo.
Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, wakati akizungumza na maofisa na askari polisi kwenye ukumbi wa mikutano wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), muda mfupi baada ya kukabidhi msaada binafsi wa magari mawili yenye thamani zaidi ya milioni 20 alioutoa kwa jeshi hilo.
Alisema wapo watu wakiwemo wafanyabiashara wakubwa wanamiliki silaha kinyume cha taratibu na inawezekana matumizi yake yakawa mabaya pia, hivyo hiyo ikawa ni moja ya sababu inayochangia kuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya uhalifu.
“RPC inakupasa kutangaza upya zoezi la uhakiki wa silaha, anzia Chunya ambako kuna machimbo ya madini, kila mwenye silaha aeleze anaimiliki kwa ajili ya shughuli gani na tuone kama vibali vyake ni halali maana wakati mwingine watu wanajisahau sana,” alisema Chalamila.
Agizo la pili, alilitaka Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na halmashauri kuhakikisha gari ndogo za kukodisha aina ya tax zinasajiliwa na kuwa na anwani ili kuondoa tax bubu kwenye maeneo yote ya mkoa huo.
Alisema agizo la tatu ni jeshi hilo kuweka mkakati wa muda mfupi wa kuruhusu magari makubwa ya mizigo na ya abiria yapite kwa awamu katika maeneo ya milima na miteremko mikali ili kupunguza ajali za barabarani ambazo ziliuandama mkoa huo siku za karibuni.
Pia aliliagiza jeshi hilo kwa kushirikiana na taasisi nyingine, kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ikiwemo ubakaji na ulawiti hasa katika Wilaya ya Chunya ambayo alidai vitendo hivyo vimekithiri.
Katika agizo lake la tano, Mkuu huyo wa mkoa aliwataka askari wa kikosi cha usalama barabarani kuwashughulikia madereva wanaokiuka sheria za usalama ikiwemo kujaza abiria kupita kiasi na kuendesha magari kwa mwendokasi bila kuchukua tahadhari.
Alisema vitendo hivyo vimeshamiri zaidi katika barabara kuu ya Mbeya – Malawi kupitia Kasumulu ambako alidai madereva wanahatarisha maisha yao na ya abiria.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alimshukuru Chalamila kwa msaada huo na kuahidi kuyatumia magari hayo kwa ajili ya kazi za doria na kukabidhiwa kwa wakuu wa polisi wa Wilaya ya Mbeya Mjini na Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi.
Jeshi la Polisi Kuanza Upya Uhakiki wa Vibali kwa Wamiliki was Silaha
0
December 07, 2018
Tags