Jinsi ya Kumtambua Mpenzi Ambaye ni Tapeli


KWENYE ulimwengu wa mahaba, wengi wanaumizwa. Wengi hufikia hatua ya kukata tamaa na kusema hawatapenda tena. Hawaoni umuhimu, wameambulia karaha za kutosha. Yote hayo hutokea kwa sababu gani? Kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye si sahihi. Asikwambie mtu, mapenzi ni matamu kama utakuwa na mtu sahihi. Inawezekana. Kwenye dunia hiihii ya matapeli wa mapenzi, wapo ambao wanajielewa. Wana nia ya dhati kabisa ya kufika mbali katika safari ya uhusiano. 

Kama wewe unahitaji kufika mbali, wapo pia wanaotamani kama wewe. Wapo wanaume wanaohitaji wanawake wa kufika nao mbali, wapo pia wanawake wanaohitaji wanaume wa kufika nao mbali. Tatizo kubwa ni watu hao kupishana. Mwanaume anapishana na mke mwema, mwanamke anapishana na mume mwema. Bahati mbaya sana, mapenzi huhifadhiwa moyoni. Ni vigumu kujua mwenzi wako anawaza nini kwenye moyo wake. Ana siri gani, anawaza nini juu yako. 

Wengi wamekuwa wajanja sana. Wanaishi na lao moyoni. Unakuwa na mtu ukiamini mpo pamoja kumbe mwenzako hayupo na wewe. Ana agenda yake binafsi. Pengine ana mtu mwingine, anampenda zaidi na wewe anakufanya kama bosheni tu. Ni hatari sana kuishi na mtu wa aina hii. Yeye anajua kupanga karata zake, anakuwa na mtu mwingine mwisho wa siku anakuja kukuacha solemba. Aliyeachwa ataumia sana. Atajutia muda alioupoteza, anayachukia mapenzi. 

UTAJUAJE ULIYE NAYE SI SAHIHI? 
Pamoja na kwamba ni ngumu sana kujua lililopo moyoni mwa mwenzako lakini kuna viashiria ambavyo unapaswa kuwa navyo makini pindi unapoviona kwa mwenzi wako. Ukiviona hivyo, fanya majaribio ya kujiridhisha, akili yako pekee inatosha kung’amua ukweli. 

KIASHIRIA CHA KWANZA 
Namna mtu anavyokutana na wewe siku ya kwanza, wakati wa mazungumzo yake ya awali utagundua ni mtu wa aina gani. Ana uharaka wa mambo? Anatumia lugha za aina gani katika mazungumzo yake? Lugha pia huweza kutoa picha ya mtu alivyo. 

Kupitia mazungumzo yake, unaweza kugundua kama ni mtu mpole. Unaweza kujua ana hekima, ana busara? Kupitia mazungumzo yake, waweza pia kujua kama ni mhuni? Waweza pia kumtambua kama hana malengo marefu. 

KIASHIRIA CHA PILI 
Baada ya kumpitisha kwenye hatua ya kiashiria cha kwanza, unashauriwa umweke karibu ili uweze kumsoma zaidi. Yawezekana akawa ameficha baadhi ya mambo katika kiashiria cha kwanza, ukamnasa katika kiashiria hiki. 

Mazungumzo yake kila wakati yanalenga kwenye hitaji fulani tu muhimu. Yawezekana akawa anahitaji fedha, anahitaji mapenzi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Ukiona mtu wa hivyo, jua kuna walakini na unaweza kumuingiza kwenye kipimo haraka na ukamtoa kabla hata moyo wako haujazama penzini. 

KIASHIRIA CHA TATU 
Hazungumzii maendeleo. Kila unapoanzisha mada ya maendeleo hususan ya uhusiano wenu, unamuona mwenzako anakupiga chenga kwa kuhamisha mada. Anatoa kipaumbele katika vitu ambavyo havina manufaa ya baadaye. 

Mambo kama matembezi, kujirusha au kwenda gesti au hotelini ndiyo anayotaka kuyasikia. Sisemi kwamba kufanya hivyo ni vibaya lakini vyote hivyo kwa mtu ambaye yupo serious, huambatana na mazungumzo ya maendeleo ya uhusiano wenu. 

KIASHIRIA CHA NNE 
Hajali. Unakuta wewe unajitoa kwa hali na mali kuhakikisha unaufanya uhusiano unakuwa hai, mwenzako hakupi ushirikiano. Yeye anakuwa na hitaji fulani tu kwako. Utahangaika kumpa zawadi mbalimbali, utamuonesha upendo wako lakini vyote hivyo mwenzako anachukulia kawaida tu. 

CHUKUA HATUA 
Ukiona mambo yanakuwa hivyo kwa muda mrefu, umeviona viashiria vyote nilivyoviainisha kwa mwenzi wako basi anza kuchukua hatua ya kumweka pembeni. Ondoa mawazo taratibu kwake, kama aliteleza bahati mbaya atarudi lakini akiendelea, jiengue utampata mwingine.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad