JPM Atoa Vitambulisho kwa Wamachinga Awatangazia Vita Mgambo

JPM Atoa Vitambulisho kwa Wamachinga Awatangazia Vita Mgambo
Rais Dkt. John Magufuli amechapisha vitambulisho 670,000 ambavyo vitagawiwa kwa wajasiriamali wadogowadogo wa mikoa yote nchini baada ya kuona mchakato wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwapatia unachukua muda mrefu tangu alipoagiza wasajiliwe ili watambulike rasmi.



Magufuli amesema hayo leo Jumatatu wakati akifungua mkutano wa TRA, wakuu wa mikoa na viongozi wa ngazi mbalimbali nchini katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.



“Agizo langu la kusajili wafanyabiashara wadogo wadogo linasuasua. Nimeona suala la vitambulisho vyao mmevichanganya na vya taifa ili tu mcheleweshe. Sasa nimetengeneza vitambulisho vyangu, vimeandikwa Kitambulisho cha Mjasiriamali, wakuu wa mikoa mtawagawia wafanyabiashara wadogo.



“Sababu nimetengeneza mwenyewe hivi vitambulisho, sioni mtu wa kumsumbua mjasiriamali. Leo nitatoa vitambulisho 25,000 kwa kila Mkuu wa Mkoa na mtavibeba kwenye magari yenu mkavigawe kwa wajasiriamali, mtawauzia kwa Tsh 20,000/=, mtazipeleka TRA na wawape risiti, tutakusanya hizi pesa ili tutengeneze vitambulisho vingine vingi zaidi.



“Mfanyabiashara mdogo mwenye mtaji chini ya Shilingi milioni 4 akiwa na kitambulisho hiki sitaki TRA, Halmashauri wala Mgambo kuwasumbua. Nawapa tu onyo msije mkachukua bidhaa za wafanyabiashara wakubwa mkawa mnawauzia ili wakwepe kodi. Niwaombe ndugu zangu wamachinga, hivi vitambulisho mvitumie vizuri na mtembee vifua mbele kama wafalme ilimradi msivunje sheria.



“Vitambulisho hivi hakuna atakayeweza kufoji, ‘never’. Najua wafanyabiashara ni wengi sana hivi ni vya kuanzia tu. Wakuu wa Mikoa wataleta idadi kamili inayohitajika ili tuchapishe vingine baada ya kupeleka return ya kadi mtakazotoa TRA.



“Kitambulisho kimoja ni Sh. 20,000/= hivyo kwa vitambulisho 25,000 itakuwa jumla ya Sh. 500,000,000/= na ipelekwe TRA ili wasije sema ni mradi wangu wakati mimi ni facilitator tu. Waambieni wasaidizi wenu wasiviuze kwa bei zaidi ya hii iliyopangwa,” amesema Magufuli.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad