Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amemsifia Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akisema kuwa ni mtu muungwana na hana unafiki na kumtaka Bernard Membe kuiga tabia hiyo.
Akizungumza jana usiku Desemba 2, 2018 mjini Geita Bashiru amesema Lowassa ambaye kwa sasa ni mwanachama wa CHADEMA, hajawahi kuzusha wala kutoa kauli mbaya dhidi ya Rais John Magufuli.
"Mtu kubaki ndani ya CCM kinafiki na kuendelea kugawa chama kwa makundi hawezi kumvumiliwa na nitahakikisha ninamaliza makundi kwenye chama", amesema Dkt Bashiru.
Kauli hiyo ya Dk. Bashiru ni mwendelezo wa mjadala kati yake na Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akimtaka afike ofisini kwake kujieleza, ambapo alitoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza akiwa mkoani Geita, akijibu ujumbe uliotumwa kwenye akaunti ya mtandaoni ya mtu mwenye jina la Bernard Membe kujibu tuhuma zilizotolewa na Dkt. Bashiru akiwa Geita.
Dkt. Bashiru alimtuhumu Membe kuandaa mpango wa kumkwamisha Rais John Magufuli katika uchaguzi wa Rais na kwamba tangu ateuliwe hajawahi kuonana na mbunge huyo wa zamani wa Mtama.
Dkt. Bashiru amesema anamheshimu Lowassa kwa uamuzi wake wa kuondoka CCM baada ya kutopewa ridhaa ya kugombea Urais na kwenda chama kingine badala ya kubaki ndani ya chama tawala kinafiki na kuwagawa wanachama
Amesema hayupo tayari kuona migogoro iliyowakumba makatibu wakuu waliomtangulia wakati wa uchaguzi akutane nayo sasa na kwamba mkakati wake mkuu ni kuua makundi.
Katibu Mkuu CCM Azidi Kumkomalia Benard Membe...Amtaka Ajifunze Toka Kwa Lowassa
0
December 03, 2018
Tags