Kauli ya NEC kwa wanaotaka kupiga kura


Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewasihi wapiga kura wote waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na wanaoishi kwenye kata 6 za Tanzania Bara, kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Jumapili Desemba 2 mwaka huu ili kuwachagua viongozi.


Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage, wakati akisoma risala ya uchaguzi mdogo wa Udiwani unaohusisha  kata za Miteja, Kivinje au Sigino , Somanga na Mitole  katika Halmashauri ya Kilwa, kata ya Muhinda katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe na Kata ya Nkoanekoli katika Halmashauri ya wilaya ya Meru. 

Wapiga Kura wapatao 31,818 wanatarajiwa kupiga Kura kuwachagua Madiwani katika Kata 6 za Tanzania Bara, na uchaguzi huo utafanyika katika vituo 91 vya kupigia kura ambako ndipo wapiga kura walijiandikishia kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015. 

“Wananchi waheshimu Sheria za Nchi wakati wote wa upigaji, kuhesabu, kujumlisha kura na kutangaza matokeo. Pale panapokuwa na malalamiko yoyote ya ukiukwaji wa sheria na taratibu za uchaguzi, yafikishwe kwenye mamlaka husika.”, Amesema Kaijage 

Jaji Kaijage aliwataka wapiga kura kuondoka kwenye maeneo ya kituo cha kupigia kura mara baada ya kupiga kura na kujiepusha na mikusanyiko au mikutano katika maeneo ya vituo vya kupigia kura kwani vyama vya siasa vimeweka mawakala vituoni ambao watalinda maslahi ya vyama husika na wagombea wao. 

“Ni wajibu wa vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia na Kujumlishia Kura kwa utaratibu ambao tulikubaliana na umekuwa ukitumika katika chaguzi" 

Maeneo mbalimbali yamekuwa yakifanya uchaguzi kutokana na sababu za viongozi wake kujiuzulu wengine kupoteza sifa za kuwa viongozi wa maeneo hayo kwa sababu za vifo au kufungwa. 

Kwenye chaguzi za marudio vyama mbalimbali vya upinzani ikiwemo CHADEMA, ACT, NCCR - Mageuzi vilitangaza kususia kwa kile ilichokidai kuwa chaguzi hizo zimekuwa haziwatendei haki.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad