Kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake wanne ya kutakatisha Dola za Marekani 173,335 imepangwa kuendelea kusikilizwa shahidi wa 10 wa Jamhuri, Januari 16, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Jana kesi hiyo ilipangwa kuendelea kusikilizwa shahidi wa 10 wa upande wa Jamhuri, lakini imeshindwa kuendelea baada ya shahidi huyo kuwa na matatizo ya kifamilia.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi, lakini shahidi waliyemwandaa amepata matatizo ya kifamilia.
Wakili wa utetezi, Richard Rweyongeza, alidai kuwa Jamhuri walitakiwa kuandaa mashahidi wawili tofauti ili mmoja anapopata tatizo au udhuru, mwingine aendelee kutoa ushahidi.
"Mheshimiwa tunaomba hili lisijirudie siku nyingine utetezi tunaomba mahakama ipange siku mbili au tatu mfululizo za kusikiliza ushahidi," alidai Rweyongeza.
Hakimu Mashauri alisema kesi hiyo itatajwa Januari 2 na kusikilizwa kwa mfululizo Januari 16, 17 na 21, 2019 na kuutaka upande wa Jamhuri uandae mashahidi wa kutosha.
Mbali na Malinzi washtakiwa wengine ni, Katibu wa zamani wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mhasibu Nsiande Mwanga, ambao wanakabiliwa na mashtaka 28 ya utakatishaji fedha.
Wengine ni Meneja, Miriam Zayumba na Karani Flora Rauya, wote wa TFF, wanakabiliwa na mashtaka 30 yakiwamo ya kula njama na kughushi.
Katika kesi ya msingi ilidaiwa kuwa Malinzi, Mwesigwa na Nsiande walitakatisha Dola za Marekani 173,335 na wako mahabusu kwa sababu mashtaka yao hayana dhamana kisheria.