Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki ameitaka mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutekeleza kiukamilifi maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzannia, Dkt John Magufuli juu ya kupunguza kodi zisizokuwa za msingi.
Kagasheki ambaye ni miongoni mwa makada wakubwa wa Chama Cha Mapinduzi, ambaye pia alihudumu kwa nafasi mbalimbali nchini ikiwemo Uwaziri pamoja na ubunge ametoa kauli hiyo baada Rais Magufuli kuitaka TRA kufanya maboresho makubwa ndani ya taasisi.
Kagasheki amesema " niombe TRA maagizo haya ya Rais myatekeleze na sio kusema “tunayafanyia kazi”, private sector yetu inadidimia biashara nyingi zimefungwa na nyingine nyingi zimehamishiwa nchi jirani. sina uhakika hii inatafsiri gani katika makusanyo yenu."
Mapema leo akizungumza na Wakuu wa Mikoa na Mawaziri na Wakuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Rais Magufuli amesema "inathibitisha kuwa ufanisi wetu kwenye ukusanyaji kodi nchini bado ni mdogo, hatutakiwi kujipongeza kwa kujilinganisha na nchi za wenzetu kama Kenya, viwango vya kodi vya nchini inawezekana viko juu ndiyo maana kuna malalamiko kwa wananchi".
"Mfano kodi ya majengo ni kubwa sana, majengo yaliyosajiliwa mpaka sasa ni milioni 1.6 napenda kurudia kodi ya majengo iwe shilingi elfu 10 kwa nyumba ya kawaida, na shilingi 20 kwa nyumba za juu na shilingi elfu 50 kwa nyumba za mjini, zitozwe kulingana na hati ya kiwanja, na si idadi ya nyumba kwenye kiwanja,"ameongeza Rais Magufuli.